Home Habari za michezo NEW STONE IMEUMALIZA MWENDO ZPL

NEW STONE IMEUMALIZA MWENDO ZPL

0

BAADA ya New Stone kutembezewa kichapo katika mechi tatu kati ya 10 zilizosalia Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), timu hiyo rasmi imeshuka daraja na msimu ujao itashiriki Ligi Daraja la Kwanza, Kanda ya Pemba.

Kati ya mechi 23 ilizocheza, imeshinda moja dhidi ya Zimamato, huku ikipoteza 22, imeruhusu mabao 66 na kufunga 15. Ina pointi tatu ikishika nafasi ya mwisho kwenye msimamo na hata ikishinda mechi zote saba zilizobaki, haiwezi kujinasua na mstari mwekundu wa kushuka daraja.

Katika mechi tatu ilizocheza hivi karibuni kabla ligi hiyo haijaenda mapumziko kwa ajili ya kupisha Kombe la Muungano, matokeo yake yalikuwa hivi; New Stone 1-3 Chipukizi, Polisi 3-1 New Stone na Mlandege 5- 1 New Stone.

Akizungumza na Soka la Bongo, Msemaji wa timu hiyo, Said Kijaji amesemaawali walikuwa na matarajio makubwa ya timu kufika mbali lakini changamoto ya ugeni ndio sababu ya kushindwa kufikia lengo hilo.

“Uzoefu umechangia kwa kiasi kikubwa timu kupata matokeo mabaya na kushuka daraja, hivyo kwasasa hatuna uwezo huo wa kubaki ligi Kuu,” alisema.

Alisema, mwanzo walikuwa na mtazamo wa kwamba baada ya kufanya vizuri Ligi Daraja la Kwanza na huko itakuwa, vivyo hivyo lakini mambo yamekuwa tofauti walichoambulia vipigo.

Amesema, awali mikakati yao ilikuwa mizuri baada kufungwa mechi tatu za mwanzo hapo ndipo walipopoteza matumaini.