Home Habari za michezo ENZO MARESCA ACHOMOZA WARITHI GUARDIOLA MAN CITY

ENZO MARESCA ACHOMOZA WARITHI GUARDIOLA MAN CITY

0

MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa zamani wa Chelsea FC Enzo Maresca ameibuka kinara katika orodha ya makocha wanaoweza kumrithi Pep Guardiola Manchester City, iwapo Mhispania huyo ataamua kuondoka mwishoni mwa msimu huu.

Guardiola, ambaye bado ana mkataba wa mwaka mmoja Etihad, ameanza kuzungumzia kwa viashiria siku zake bora City zinaweza kuwa zinakaribia ukingoni, jambo lililoweka klabu hiyo kwenye mpango wa kujipanga upya mapema.

Maresca, ambaye hana kazi tangu Januari mwaka huu baada ya kuondoka Chelsea, sasa anatajwa kuwa jina linalopigiwa hesabu kubwa na bodi ya Man City pamoja na idara ya ufundi inayoongozwa na Hugo Viana.

Ripoti zinaeleza kocha huyo amekuwa akijadiliwa katika vikao vya ndani kutokana na uelewa wake wa falsafa ya Guardiola.

Hata hivyo, changamoto kubwa inabaki kuwa mkataba wake na Chelsea wa miaka mitatu na nusu, jambo linaloweza kufanya uhamisho wake kuwa mgumu iwapo City wataamua kumchukua.

Kabla ya kuondoka Chelsea, Maresca aliripotiwa mara mbili kufanya mazungumzo ya awali na baadhi ya maofisa wa City kuhusu uwezekano wa kumrithi Guardiola, taarifa iliyozua mjadala mkubwa England. Aliondoka Stamford Bridge Januari akiwa kwenye maandalizi ya kukutana na City katika Uwanja wa Etihad, hatua iliyowashangaza wengi.

Guardiola mwenyewe aliwahi kumpongeza kwa kusema: “Enzo ni mmoja wa makocha bora duniani. Kazi aliyoifanya Chelsea ni ya kipekee.” Wawili hao wana historia ya kufanya kazi pamoja City, ambapo Maresca alikuwa msaidizi wake wakati wa msimu wa 2023 uliomalizika kwa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

City kwa sasa inaongoza Ligi Kuu England ikiwa katika mbio kali na Arsenal, huku mustakabali wa Guardiola ukiendelea kuwa mada kubwa ndani ya klabu hiyo ambayo imeshinda mataji 18 chini yake.

Mwaka 2024, Maresca aliiongoza Leicester City kubeba ubingwa wa Championship kabla ya kuelekea Chelsea, ambako alifuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya na kushinda Conference League pamoja na Kombe la Dunia la Klabu katika msimu wake wa kwanza, kabla ya matokeo kuyumba baadaye.