UONGOZI wa Simba SC umeweka wazi sababu ya kuhamishia mchezo wa Kariakoo Derby katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, ukieleza kuwa uamuzi huo umetokana na Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, kuwa kwenye matengenezo kwa ajili ya maandalizi ya AFCON 2027.
Awali, dabi hiyo kubwa iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi ilipangwa kuchezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa. Hata hivyo, kutokana na maboresho yanayoendelea uwanjani hapo, mechi hiyo sasa itapigwa Mei 3, 2026 katika dimba la Meja Jenerali Isamuhyo lililopo Mbweni.
Akizungumza kuhusu mabadiliko hayo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema kuwa licha ya Meja Jenerali Isamuhyo kuwa uwanja wa nyumbani wa timu hiyo kwa msimu huu, bado walikuwa na dhamira ya kuutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya Kariakoo Derby.
Ameeleza kuwa kulikuwa na makubaliano ya pamoja kati ya vilabu, mamlaka za mpira pamoja na serikali kwamba michezo mikubwa nchini, ikiwemo Kariakoo Derby, ipigwe katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kutokana na hadhi yake na uwezo wake wa kuchukua mashabiki wengi.
Kwa mujibu wa Ahmed Ally, Simba ilifuata taratibu zote kwa kuwasilisha maombi rasmi kwa wamiliki wa uwanja huo ikiomba ruhusa ya kuutumia kwa ajili ya dabi hiyo. Hata hivyo, walipokea majibu kuwa kwa sasa uwanja huo haupatikani kutokana na kuendelea na ukarabati mkubwa unaolenga kuuboresha kuelekea AFCON 2027.
Kutokana na hali hiyo, Simba walilazimika kufanya uamuzi wa kutafuta uwanja mbadala, ambapo hatimaye walichagua Meja Jenerali Isamuhyo, ambao wamekuwa wakiutumia tangu kuanza kwa msimu huu, ili kuhakikisha mchezo huo muhimu unafanyika bila kuathiri ratiba