Home Habari za michezo NJIA YA FAINALI YAPITIA KWA AZAM FC, YANGA YAPANIA KUPENYA

NJIA YA FAINALI YAPITIA KWA AZAM FC, YANGA YAPANIA KUPENYA

0

NYASI za Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, leo saa 2:15  zitawaka moto zitakapokutanisha wapinzani wawili Yanga dhidi ya Azam FC katika mchezo wa nusu fainali ya kombe la Muungano.

Nusu fainali hiyo ya kwanza na mshindi wa mchezo huo ataenda kukutana na mshindi kati ya nusu fainali ya pili kati ya Simba au Mlandege SC.

Kuelekea mchezo huo kocha wa Yanga,  Pedro  Gonçalves, amesema timu yake inatarajia kukutana na upinzani mkali kutoka kwa Azam FC katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Muungano utakaopigwa hivi karibuni.

Amesema  Azam FC ni timu yenye ubora mkubwa na wachezaji wenye uwezo, hali inayowafanya kujiandaa kwa umakini mkubwa kuelekea mchezo huo.

“Tunatambu ugumu wa mechi hiyo, tumeweka mikakati madhubuti kuhakikisha tunapata ushindi,” amesema kocha huyo.

Ameongeza kuwa licha ya ratiba kuwa ngumu kutokana na michezo ya ligi inayoendelea, kikosi chake kimeendelea kufanya maandalizi kwa umakini mkubwa.

Amesema wachezaji wako katika hali nzuri ya ushindani na wana ari ya kupambana ili kufikia malengo yao ya kutinga fainali.

Amesema  mechi hiyo ni muhimu kwa timu yake, kwani ushindi utawapa nafasi ya kusogea hatua ya mwisho ya mashindano hayo ikiwemo kucheza fainali na kutwaa kombe la Muungano.

Kocha huyo amewataka wachezaji wake kucheza kwa nidhamu, umakini na kujituma kwa hali ya juu ili kuhakikisha wanapata matokeo chanya.

Mchezo huo wa nusu fainali unatarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi wa soka, huku kila timu ikipania kuonyesha kiwango bora uwanjani. Ushindani mkubwa unatarajiwa kutokana na ubora wa vikosi vya timu zote mbili.