Home Habari za michezo YANGA YAIKIMBIA SIMBA WAITAKA MLANDEGE

YANGA YAIKIMBIA SIMBA WAITAKA MLANDEGE

0

WAKATI presha ya kuelekea fainali ya Kombe la Muungano ikiendelea kupanda, vita ya maneno kati ya watani wa jadi, Simba na Yanga, imeanza kuchukua sura mpya.

Hii ni baada ya Yanga kuonekana kugeuza mwelekeo wa matarajio yao ya fainali kwa kutotaja wazi nia ya kukutana na Simba, badala yake wakionesha kuvutiwa zaidi na Mlandege SC.

Kauli hiyo imekuja muda mfupi baada ya Simba kuweka wazi kupitia Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally, kwamba wao wanaitamani Yanga kwenye mchezo wa fainali.

Kauli ya Simba ilikuwa wazi ikionesha kiu ya kukutana na watani wao wa jadi ili kuamua ubabe, jambo lililoongeza hamasa kwa mashabiki wa soka nchini.

Hata hivyo, upande wa Yanga mambo yanaonekana kwenda tofauti. Msemaji wa klabu hiyo, Ali Kamwe, ameibuka na kauli iliyoibua mjadala mkubwa, akionesha wazi kuwa anatamani kuona Yanga ikikutana na Mlandege SC kwenye hatua ya mwisho ya mashindano hayo badala ya Simba.

Akizungumza kwa mtindo wa mzaha uliojaa ujumbe mzito, Kamwe alisema kuwa mashindano hayo yamekosa ladha kutokana na ukosefu wa mvutano wa kawaida wa watani wa jadi.

Amedokeza kuwa yupo tayari kurejea na kushuhudia fainali kati ya Yanga na Mlandege, akionesha wazi ni upande gani anaona ungekuwa bora kwake.

Wakati kauli hiyo ikiendelea kuzua tafsiri tofauti kwa mashabiki na wadau wa soka, Yanga yenyewe inatarajiwa kushuka dimbani leo usiku kuikabili Azam FC katika mchezo wa nusu fainali utakaopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. Huu ni mtihani muhimu kwa Yanga kuthibitisha kama wanaweza kufika hatua ya fainali.

Kwa upande mwingine, kauli ya Kamwe imechukuliwa na baadhi ya mashabiki kama ishara ya tahadhari au mbinu ya kisaikolojia kuelekea michezo mikubwa, wengine wakiamini ni njia ya kupunguza presha ya mapema ya Kariakoo Derby inayoweza kutokea fainali.