KOCHA mkuu wa Pamba Jiji, Francis Baraza, amesema matokeo ya hivi karibuni ya Fountain Gate yameanza kumpa wakati mgumu kuelekea mchezo ujao akimtaja kocha Fredi Felix ‘Minziro’ kuwa amewafanya wapinzani wao hao kuanza kuwa bora.
Pamba Jiji imetoka kupata matokeo yasiyoridhisha katika mechi nne mfululizo, huku ikipoteza mbele ya Yanga 0-3 na kutoka na sare mara tatu. Mchezo unaofuata itakutana na Fountain Gate iliyotoka kuichapa Mtibwa Sugar 2-1, huku matokeo yao yakiwa nuru mpya baada ya kupoteza mechi 10 kati ya 19.
Akizungumza na Mwanaspoti, Baraza amesemakiwango walichoanza kukionesha wapinzani wao kinaongeza ushindani mkubwa.
Amesemakuwa ushindi walioupata umebadilisha taswira ya timu hiyo na umebadili kabisa mipango na maandalizi ya kikosi hicho.
“Kwa sasa naiongezea nguvu zaidi timu hasa kwenye maeneo mawili, pumzi na stamina, lakini pia nitahakikisha tunakuwa na mbinu za kuwafanya Fountain wafanye makosa ili tupate ushindi.
“Najua wapi pa kuwashika wapinzani wetu, tunajiamini kwa uzoefu tulionao ndio utakaotusaidia kuusoma mchezo kwa haraka na kuwadhibiti.”
AMGUSA MINZIRO
Ikumbukwe Fountain ilimtangaza kocha mpya, Fredi Felix ‘Minziro’, Aprili 10, 2026 ambaye ni mrithi wa Mohamed Laizer aliyeondolewa.
Minziro mpaka sasa ameiongoza timu hiyo kwenye mechi tatu dhidi ya Azam na Simba ambako alifungwa mabao 7-0, huku akiambulia pointi tatu dhidi ya Mtibwa.
Baraza amesemaanamjua Minziro ni miongoni mwa makocha wazuri wenye uwezo mkubwa anayejua kuitengeneza timu kwa haraka.
“Najua falsafa za kocha Minziro, ni mwalimu ambaye ana uwezo wa kuibadilisha timu ikafanya makubwa kwa muda mfupi kutokana na uzoefu alionao,” amesema.
Minziro pia aliwahi kuinoa Pamba Jiji msimu uliopita kabla ya kutimkia Mashujaa FC, kabla ya kujiunga na Fountain Gate.






