Home Habari za michezo WAPEWE DABI, REKODI HISTORIA ZINAWABEBA WAAMUZI HAWA

WAPEWE DABI, REKODI HISTORIA ZINAWABEBA WAAMUZI HAWA

0

LIGI Kuu Bara imesimama kupisha michuano ya Kombe la Muungano inayoendelea visiwani Zanzibar na licha ya mashabiki kufuatilia timu zao huko, akili zao pia zipo kwenye mechi ya ‘derby’ baina ya Simba na Yanga itakayopigwa Mei 3.

Mechi ya watani inafuatiliwa na mashabiki wengi ndani na nje ya nchi na kwa sasa vijiweni tambo zinatawala, huku shauku kubwa ni kujua itapigwa wapi kwani bado uwanja haujatangazwa na mwamuzi gani atasimamia mechi hii ambayo husimamisha shughuli kupisha kuona wababe hao wa Kariakoo wakipambana kwa dakika 90.

Ligi Kuu Bara imeshuhudia waamuzi wengi wakichezesha mechi za dabi tangu kuanza kwa ligi hii na wapo waliomaliza salama na kupata sifa na wapo waliojikuta wakiadhibiwa kutokana na kushindwa kumudu kutafsiri sheria 17 za soka.

Wapo waliofungiwa na waliosimamishwa hivi karibuni kutokana na makosa kama hayo huku baadhi ya timu zikinufaika na maamuzi yao na wapo ambao tangu kuanza kwa msimu wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la CRDB hawajawahi kukumbana na adhabu yoyote wala malalamiko kutoka kwa wachezaji, viongozi wa timu na hata mashabiki. Kwa kifupi, hata Kamati ya saa 72 haijawahi kuwaita kwa sababu wameonyesha ubora na uwezo katika kuzitafsiri sheria za soka katika dakika 90 za mechi.

Baadhi ya waamuzi wazoefu katika kusimamia mechi za dabi ni Heri Sasii, Ahmed Arajiga, Ramadhan Kayoko na Nassor Mwinchui na wengine ingawa wapo ambao wameonja rungu la kamati hiyo kwa kufungiwa na kuondolewa kwenye orodha.

Hata hivyo, msimu huu, wapo ambao licha ya kutokuwa na uzoefu mkubwa na hawajawahi kuchezesha mechoi ya Dabi ya Kariakoo, wameonyesha uwezo mkubwa na rekodi zao zimewafanya kukubalika na wadau na mashabiki na wanashawishi kukabidhiwa kipyenga Mei 3.

WILSON MASEA

Alianza kazi ya uamuzi wa soka mwaka 2012 akichezesha ligi za wilaya, jijini Mwanza. Ni mmoja wa waamuzi ambao hawapepesi macho kazini katika kusimamia sheria na kanuni za mchezo huo.

Ni mpole na mwenye uweledi akiwa katika majukumu yake na hilo limemfanya kuwa mmoja wa waamuzi ambao katika mechi alizosimamia kutokuhojiwa na Kamati ya saa 72, kulaumiwa na wachezaji na hata mashabiki.

Mechi alizochezesha msimu huu ni KMC dhidi ya Mbeya City, Singida dhidi ya Coastal Union, Tanzania Prisons dhidi ya Yanga, TRA United dhidi ya KMC, Yanga dhidi ya Mbeya City na Pamba dhidi ya Namungo.

Pamoja na matokeo ya mechi hizo, hakukuwapo na malalamiko kutoka kwa wachezaji, timu wala mashabiki na hivyo, msomi huyu wa shahada ya ualimu katika masomo ya Hisabati na Fizikia ni mmoja wa waamuzi ambao wakipewa mechi hiyo ya dabi, huenda wakawa na imani naye.

SIFU AMON

Anatoka jijini Mbeya na amekuwa na uwezo mkubwa katika kusimamia mechi za ligi na Kombe la Shirikisho la CRDB, akizingatia sheria na kanuni za soka.

Hadi sasa amesimamia mechi 10 na zote hakujatokea malalamiko wala kuitwa na Kamati ya saa 72 na licha ya kutokuwa na uzoefu mkubwa akianza kazi hiyo mwaka jana, ameonyesha nidhamu, akiendana na kasi ya mechi na hivyo kuifanya kazi yake kuwa nyepesi.

Mechi alizochezesha ni KMC dhidi ya Singida Black Stars, JKT Tanzania dhidi ya Mtibwa Sugar, Simba dhidi ya Mtibwa Sugar, Mtibwa Sugar dhidi ya Coastal Union na Azam dhidi ya TRA United.

Nyingine ni Namungo dhidi ya JKT Tanzania, Pamba dhidi ya Yanga kwa upande wa Ligi Kuu, huku za kombe la shirikisho ni Namungo dhidi ya Kagera Sugar na Simba dhidi ya Dodoma Jiji hatua ya robo ya 16 bora.

Kutokana na kuaminiwa kwake na kuonyesha uwezo katika mechi hizo 10, zikiwamo kubwa, ni wazi akipewa mechi ya dabi ataimudu kwa dakika zote 90.

SAAD MROPE

Tangu alipomaliza kozi yake mwaka 2014 na kuanza kuliamsha mwaka 2015, amekuwa na ubora huku wadau na mashabiki wa soka wakikubali shughuli yake.

Mrope ambaye pia ni inspekta wa Jeshi la Polisi, Dodoma, pia ni msomi mwenye Shahada ya Elimu ya Viungo na Sayansi ya Michezo na anayamudu majukumu yake vyema nje na ndani ya uwanja.

Msimu huu amechezesha mechi saba bila ‘makosa ya kibinadamu’ na amekuwa kipenzi cha mashabiki kutokana na kutenda haki muda wote bila upendeleo wala kuonea upande wowote katika mechi.

Mechi zaka hadi sasa raundi 19, ni Coastal Union dhidi ya JKT Tanzania, Mbeya City dhidi ya Tanzania Prisons, Pamba Jiji dhidi ya Azam FC, Yanga dhidi ya JKT Tanzania, TRA United dhidi ya Namungo, Yanga dhidi ya Tanzania Prisons na Fountain Gate dhidi ya Simba.

KAULI ZA WADAU

Mdau wa soka kutoka mkoani Songwe, Moses Charles anasema kwa sasa waamuzi wengi wameonekana kuwa imara uwanjani kutokana na mamlaka za soka kutowafumbia macho wale wanaoboronga.

Anasema katika kukuza na kutanua wigo wa waamuzi, shirikisho la soka nchini linaweza kuwapa waamuzi ambao wanajitafuta na kuondoa dhana ya kuwapanga waliozoeleka.

“Kuna kipindi waliletwa waamuzi kutoka nje lakini siioni kama ni bora ilhali tunao waamuzi wenye uwezo na elimu, mtu akifanya vizuri apongezwe na kuaminiwa. Waamuzi chipukizi wanafanya vizuri,” anasema Charles.

“Mimi binafsi nashauri watafute waamuzi ambao hawana vinasaba vya Simba na Yanga, wanaotimiza wajibu wao kwa mujibu wa kanuni na sheria za soka bila kupendelea au kuonea, tumeona mara kadhaa maamuzi ya upande mmoja kwenye hizi dabi.”

Kwa upande wake, Yusuph Edson anasema wapo waamuzi wengi msimu huu wameonyesha uwezo na weledi katika kusimamia kanuni za soka akiomba uwezekano wa kuwapa nafasi ili kuonesha uwezo wao.

“Ligi si ya timu moja wala refa mmoja, tunaona hata kwa wenzetu Ulaya refa akiwa na sifa anapewa jukumu kuchezesha mechi yoyote, kwetu sisi tunaona kila mara mtu yuleyule, hii inaweza kutupa maswali mengi,” anasema Edson.