Vita nyingine itakuwa eneo la kiungo ambapo endapo Fei Toto atakuwa uwanjani anayeongoza kwa asisti kule ligi kuu akiwa nazo saba, basi kuna uwezekano watakumbushia tena mbio zao za kutengeneza asisti kati yake na Allan Okello wa Yanga ambaye kwenye mashindano haya tayari anayo moja. Kwenye ligi anazo sita, moja nyuma ya Fei Toto.
Kwa Yanga, Duke Abuya, Mudathir Yahya, Mohamed Damaro na Maxi Nzengeli wanatarajiwa kuongoza eneo la kati.
Azam chini ya Ibenge, tunaweza kuona sapraizi huenda atampa nafasi Adolf Mtasingwa ambaye sasa yupo fiti baada ya kupona majeraha na tayari amecheza dhidi ya KVZ, pia mkata umeme mwingine, Sadio Kanoute yupo tayari kwa mapambano.
Kwa ubora wa majina haya, eneo la kiungo linaonekana kuwa uwanja wa mapambano makali kati ya wakabaji na watengenezaji wa mashambulizi, hali itakayoweza kuamua matokeo ya mechi.
WASIKIE WENYEWE
Kocha wa Azam, Florent Ibenge alisema:
“Kesho (leo) ni mchezo mkubwa kila mmoja anajua kwa sasa kwenye ligi yetu kule Yanga ndio timu bora kwa takwimu, sisi Azam tunafahamu tunakwenda kukutana na timu ngumu yenye hadhi hiyo kwenye mchezo wa nusu fainali,” amesemaIbenge.
“Sisi (Azam) tunapenda kucheza mechi ngumu kama hizi, nawapongeza sana wachezaji wangu kwa kujituma na kufikia hatua hii, tumejiandaa kucheza kama ambavyo tumekuwa tukicheza, tutawapa nafasi wachezaji ambao tunaamini wataweza kutupa matokeo mazuri, najivunia wachezaji wangu haijalishi ni vijana au wale wakongwe.”
Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves alisema:
“Kesho (leo) ni nusu fainali tutakutana na Azam FC, moja ya timu bora zinazowania mataji hapa Tanzania, ni timu yenye nguvu, iliyofanya uwekezaji mkubwa, wanaohtaji mashindano kama haya kuthibitisha ubora wao, yenye wachezaji wazuri na kocha mwenye wasifu mkubwa kwenye soka la Afrika,” amesemaGoncalves.
“Tunatarajia mchezo mgumu, tunatakiwa kuwa tayari kukabiliana nao, tunapita kwenye ratiba ngumu ya mashindano, sasa tuna mchezo wa nusu fainali na baada ya hapo tukishinda tutakwenda kwenye fainali tukimaliza mashindano haya tutakuwa na mchezo mgumu wa ligi dhidi ya Simba, lakini ni motisha kwetu kucheza dhidi ya wapinzani wetu wakubwa, tukiwa na akili ya kushinda hizo mechi.”