BAADA ya Yanga kufanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Muungano, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, ameibuka na kauli ya kuonyesha furaha yake akisema, “Hii ndiyo tulivyokuwa tunaitaka.”
Kauli hiyo inaashiria wazi kuwa Simba wamekuwa na shauku ya kukutana na watani wao wa jadi, Yanga, katika hatua ya fainali ya michuano hiyo mikubwa ya Muungano.
Ni kauli iliyochochea hamasa kwa mashabiki wengi wa soka ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakisubiri pambano hilo la dabi.
Wakati Yanga tayari wameshakata tiketi ya fainali, Simba wao wanakabiliwa na kibarua kigumu leo jioni katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Mlandege SC utakaochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar.
Iwapo Simba watafanikiwa kushinda mchezo huo, watakutana na Yanga katika fainali inayosubiriwa kwa hamu kubwa na wadau wa soka nchini, ikiwa ni mechi itakayowakutanisha mahasimu hawa kabla ya dabi nyingine ya Ligi Kuu Tanzania Bara inayotarajiwa kuchezwa Mei 3, 2026.
Kwa mujibu wa Ahmed, Simba walikuwa na tamanio la dhati la kukutana na Yanga katika fainali hiyo, na sasa wanaamini ndoto yao iko karibu kutimia.
Amesisitiza kuwa kikosi hicho kitaingia uwanjani kwa nguvu zote kuhakikisha kinapambana vikali dhidi ya Mlandege SC ili kufanikisha lengo hilo.