KOCHA Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema hawezi kubashiri kwa uhakika ni timu gani itaibuka mshindi katika mchezo wa nusu fainali kati ya Simba na Mlandege SC, akisisitiza kuwa mpira wa miguu una matokeo yasiyotabirika.
Pedro ameweka wazi kuwa kikosi chake kipo tayari kukutana na timu yoyote itakayofanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Muungano, iwe ni Simba au Mlandege SC, huku akieleza kuwa maandalizi yao yako imara kwa ajili ya pambano hilo kubwa.
Yanga tayari imefanikiwa kufuzu hatua ya fainali na sasa inasubiri mshindi wa nusu fainali ya pili kati ya Simba na Mlandege SC, mchezo utakaopigwa jioni ya leo kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Kocha huyo ameongeza kuwa endapo Simba wataibuka na ushindi, basi fainali hiyo itakuwa na ladha ya kipekee kutokana na uwepo wa dabi ya Kariakoo, jambo litakaloongeza ushindani mkubwa pamoja na presha kwa timu zote mbili kutokana na kukutana mara mbili ndani ya muda mfupi.
“Malengo ya Yanga hayabadiliki, tunataka kufika fainali na hatimaye kutwaa ubingwa,” amesema Pedro.
Amesisitiza umuhimu wa maandalizi sahihi, nidhamu kwa wachezaji na umakini katika kutumia nafasi watakazopata uwanjani ili kufikia malengo hayo.
Pedro pia amebainisha kuwa kikosi chake kina ari kubwa ya ushindi na kimejipanga kikamilifu kuhakikisha kinatimiza malengo yao, huku akiwataka mashabiki kuendelea kutoa sapoti katika hatua hizi muhimu za mashindano.