Home Habari za michezo ROMMY3D AFICHUA NUMA YA TALAKA YA TARAKA YAKE KWA SHILOLE

ROMMY3D AFICHUA NUMA YA TALAKA YA TARAKA YAKE KWA SHILOLE

0

MPIGA picha maarufu nchini, Rajabu Issa ‘Rommy3D’, amefunguka kuhusu kile kilichojificha nyuma ya talaka yake na msanii, Zuwena Mohamed ‘Shilole’, akieleza namna alivyojikuta kwenye kipindi kigumu zaidi cha maisha yake ndani ya muda mfupi baada ya ndoa hiyo kuvunjika.

Aprili 22, 2021, Shilole alifunga ndoa na Rommy3D ambapo walidumu kwa takribani miaka mitatu hadi Mei 28, 2024 ilipotoka taarifa ya kuachana kwao ambapo hivi sasa kila mmoja anaendelea na maisha yake.

Akizungumza na Soka la Bongo, Rommy3D amesema talaka hiyo haikuwa tu mwisho wa ndoa yake bali pia mwanzo wa changamoto nzito ambazo hakuwahi kuzitarajia, akidai hakuwa amejiandaa kisaikolojia kuanza maisha mapya bila mwenza wake.

Ameeleza kuwa, uamuzi wa kutangaza talaka kupitia mitandao ya kijamii ulikuwa wa makusudi kabisa, ukiwa na lengo la kufunga mjadala wa uwezekano wa maridhiano, huku akifichua kwamba, alianza kutoa talaka halafu akaenda kuandika mtandaoni.

“Watu wengi hawajui kilichofanyika, wanasema tu nimetoa talaka mtandaoni, mimi nilianza kutoa talaka kwanza, halafu ndio nikaenda kuandika mtandaoni, na nilifanya vile ili nipigilie msumari. Sikupenda kuona kuna nafasi ya watu kuanza kunishawishi nirudiane. Nilitaka kila kitu kiishe mara moja.

“Chanzo cha ndoa kuvunjika ni usaliti na marafiki, sababu marafiki ambao walikuwa wanakuja kuniambia vitu vya Shilole, wanatoka hapo wanaenda pia kumwambia Zuwena (Shilole) vitu vyangu, sasa ikawa sisi ndani ya nyumba tunawindana, ndipo siku moja Juma Lokole aliposti picha Zuwena akiwa na mchumba wake wa sasa hivi, nami nikaona hapa hapa nisikawie kutoa talaka,” amesema Rommy3D.

Kwa mujibu wa mpiga picha huyo, alihofia kuwa ndugu na marafiki wangeingilia kati na kuanzisha mazungumzo ya siri ya kuwapatanisha, jambo ambalo hakulitaka kabisa kwa wakati huo.

Mbali na maumivu ya kuvunjika kwa ndoa, Rommy3D alikumbana na pigo jingine kubwa ndani ya wiki hiyo hiyo, studio yake iliharibiwa vibaya na mvua kubwa iliyonyesha, hali iliyosababisha kupoteza vifaa muhimu vya kazi ikiwemo kamera na kompyuta.

Amesema tukio hilo lilimvuruga zaidi kisaikolojia, kwani alipoteza vitu viwili muhimu kwa wakati mmoja, ndoa yake na msingi wa kipato chake.

“Kilikuwa kipindi kigumu sana. Ndani ya wiki moja nimeachana na mke wangu, halafu mvua kubwa ikanyesha na kuingia studio na kuharibu kila kitu. Nilihisi kama nimepoteza kila kitu kwa mpigo,” amefafanua.

Hata hivyo, Rommy3D aliwashukuru marafiki zake waliomsimamia katika kipindi hicho kigumu, akisema msaada wao ulimuwezesha kusimama tena na kuanza kujijenga upya hadi kufikia hali aliyonayo sasa.

“Nimekaa mwaka mmoja na nusu bila ya kuwa na ofisi, nimekuwa mtu wa kwenda kwenye ofisi za watu na kuanza kuomba kufanyia kazi, ila muda sio mrefu nitafungua ofisi Sinza, nimeshaanz maandalizi,” amesema Rommy3D.