MSANII mkongwe wa muziki wa Bongo Fleva, Sefu Shabani ‘Matonya, ametoa kauli nzito akisisitiza kuwa, kutokana na kile kinachomkabili, hataki kabisa kuzungumziwa na mtu yoyote, zaidi akisisitiza atakuja kuzungumza mwenyewe.
Matonya, ameeleza kwamba, hivi sasa anakabiliwa na changamoto nzito zinazohitaji utulivu na faragha zaidi kuliko kelele za nje, hivyo aachwe kwanza.
Kupitia mawasiliano ya simu yaliyonaswa na Simulizi na Sauti (SnS), Matonya ambaye kwa sasa anazuiliwa na polisi katika jiji la Mombasa nchini Kenya kwa tuhuma za ubakaji, alisikika akizungumza kwa sauti ya uchovu na kusisitiza kuwa hataki mtu yeyote, iwe ni rafiki, shabiki au hata ndugu wa karibu kutoa maoni au kumsemea kuhusu sakata lake hilo.
Katika mazungumzo hayo na D Rash The Baddest, msanii huyo ameonyesha wazi kuwa anahitaji muda wa kukabiliana na hali yake binafsi bila presha ya mijadala ya umma.
“Nisingependa kabisa mtu yeyote anizungumzie kwa sasa. Tayari nipo kwenye matatizo na sitaki kabisa kuongezewa mzigo mwingine. Kama nitakuwa na jambo la kusema, nitajitokeza mwenyewe na kulieleza. Tafadhali naomba kila mtu aheshimu hilo hata mama yangu mzazi asinizungumzie,” amesema Matonya.
Kwa upande mwingine, D Rash The Baddest ameeleza kuwa, juhudi za kuhakikisha msanii huyo anapata msaada wa kisheria zinaendelea kuchukuliwa kwa uzito, akibainisha kuwa timu inayoshughulikia suala hilo ina matumaini kuwa mchakato wa dhamana unaweza kukamilika mapema, huku uwezekano wa kuachiwa ukitajwa kuwa ni Jumatatu ijayo endapo kila kitu kitaenda kama kilivyopangwa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Kenya, Alhamisi ya Aprili 9, 2026, Matonya alifikishwa mahakamani katika eneo la Shanzu, Kaunti ya Mombasa nchini Kenya akikabiliwa na shtaka la ubakaji.
Daily Nation imeripoti kuwa, upande wa mashtaka uliieleza mahakama kuwa Aprili 7, 2026, katika Jengo la Josy Joka Apartments lililopo Nyali, msanii huyo anadaiwa kumuingilia kimwili mwanamke aliyetajwa katika nyaraka za mahakama kwa herufi J.G kwa kutumia nguvu.
Sakata hili limekuwa gumzo kubwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania, hasa kutokana na uzito wa tuhuma hizo pamoja na historia ya msanii huyo kwenye tasnia ya muziki.
Wengi wanakumbuka kuwa Matonya aliwahi kujizolea umaarufu mkubwa kupitia nyimbo zake kama Vaileti, Anita na Spair Tairi, kabla ya kupotea kwa muda mrefu kwenye ramani ya muziki, hivyo kurejea kwake kulitarajiwa kuleta ushindani mpya lakini badala yake, amejikuta katikati ya kesi inayoweza kuathiri kwa kiasi kikubwa maisha yake ya kazi na taswira yake kwa umma.
Kesi hiyo imepangwa kutajwa tena Aprili 30, 2026 kwa ajili ya maandalizi ya awali kabla ya kuanza kusikilizwa rasmi.