Home Habari za michezo SIKINDE, BOGOSS MUSICA KUTIKISA FAINALI YA CHEZA KIDANSI AWARDS

SIKINDE, BOGOSS MUSICA KUTIKISA FAINALI YA CHEZA KIDANSI AWARDS

0

IJUMAA hii katika eneo la Ngoreme Park Sinza Mori jijini Dar es Salaam, mashabiki wa muziki wa dansi wanatarajiwa kushuhudia kilele cha msimu wa saba wa tuzo pekee za muziki huo hapa nchini, Cheza Kidansi Music Awards, tukio litakalojumuisha ugawaji wa tuzo na burudani ya nguvu kutoka kwa bendi mbalimbali.

Katika usiku huo wa kihistoria, Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde Ngoma ya Ukaye’ chini ya Ramdhani Mapesa, wataweka burudani ya aina yake, huku Bogoss Musica chini ya uongozi wa Nyoshi El Saadat wakitarajiwa kupagawisha mashabiki kwa mitindo yao ya kipekee ya dansi.

Tuzo hizo ambazo zimekuwa zikikua mwaka hadi mwaka, zinaandaliwa na kampuni ya Cheza Kidansi Entertainment chini ya mwandaaji na mwanahabari mbobevu wa muziki wa dansi, Bernard James, ambaye amesema maandalizi yako katika hatua za mwisho kuhakikisha mashabiki wanapata burudani bora.

Akizungumza kuelekea fainali hiyo, Bernard James amesema: “Cheza Kidansi Music Awards zimekuwa hazina ya muziki wa dansi nchini. Lengo letu ni kuhakikisha tunalinda na kukuza muziki huu kwa kuwapa wasanii jukwaa la heshima na ushindani wa haki. Nawakaribisha wadau wote kujitokeza kwa wingi Ngoreme Park kuunga mkono tasnia yao.”

Kwa upande wake, Nyoshi El Saadat, amesema kuwa ushiriki wa Bogoss Musica kwenye fainali hiyo ni nafasi muhimu ya kuonesha ubora wa bendi yao mbele ya mashabiki na wadau wa muziki.

“Tunaamini hii ni hatua kubwa kwetu, tumejiandaa kuhakikisha mashabiki wanapata burudani ya kiwango cha juu, dansi ni maisha yetu, na tutahakikisha tunawapa watu kile wanachokitarajia,” amesema Nyoshi El Saadat.

Kwa upande wa Sikinde Ngoma ya Ukaye, Ramadhani Mapesa, ameweka wazi kuwa bendi yao imejiandaa kikamilifu kuendeleza historia ya muziki wa dansi kwa kutoa burudani itakayowakumbusha mashabiki ladha ya asili ya muziki huo.

Tuzo hizi zimeendelea kuimarika kila mwaka, sasa zimekuwa sehemu muhimu ya kalenda ya burudani nchini.

Bernard James ameongeza kuwa, mshikamano wa wadau ndio utakaofanikisha zaidi ukuaji wa tuzo hizo.

“Tunawahitaji sana wasanii na wadau wote. Hii siyo tuzo ya mtu mmoja, ni ya tasnia nzima ya muziki wa dansi. Tukishikamana, tunaweza kufika mbali zaidi,” amesema.

Wito umetolewa kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi Mei Mosi mwaka huu pale Ngoreme Park, kununua tiketi na kushuhudia kilele hicho cha burudani ambacho kinatarajiwa kuwa cha aina yake katika kalenda ya muziki wa dansi nchini.