LONDON, ENGLAND: ALIYEKUWA kipa wa Tottenham Hotspur, Alfie Whiteman, ameanza maisha mapya nje ya soka akiwa mkurugenzi wa filamu, mwigizaji, dijei (DJ) na mpiga picha baada ya kustaafu mchezo huo akiwa na umri wa miaka 26.
Whiteman alikuwa sehemu ya kikosi cha Tottenham kilichotwaa Europa League mwaka jana mjini Bilbao, ingawa alisugua benchi.
Chini ya mwaka mmoja baada ya mafanikio hayo, sasa ni dijei ndani ya uwanja wa klabu hiyo, Tottenham Hotspur.
“Sikuwahi kupanga watu waone picha hizi. Inaonyesha namna nilivyokuwa naishi maisha yangu kama niliyagawanya mara mbili,” amesema.
Baada ya zaidi ya miaka 15 akiwa Tottenham tangu alipokuwa na miaka 10, Whiteman alichukua uamuzi mgumu wa kuachana na soka licha ya kuwa bado na uwezo wa kucheza kwa muda mrefu zaidi.
“Ni kama kuachana na ndoto ya utotoni. Lakini miezi nane iliyopita imekuwa bora zaidi maishani mwangu,” amesema.
Licha ya kupata ofa kutoka klabu za Championship na League One, aliamua kuwekeza nguvu zake kwenye sanaa na ubunifu.
Wakati akiwa mchezaji, Whiteman alikuwa akiishi maisha tofauti na wachezaji wengi. Alikuwa akikutana na waongozaji wa filamu, kufanya kazi kama msaidizi wakati wa kurekodi na hata kujifunza uigizaji.