SIMBA SC wamehitimisha kwa kishindo michuano ya Kombe la Muungano, si tu kwa kutwaa ubingwa bali pia kwa kutikisa jukwaa la tuzo kwa kuvuna jumla ya tuzo tano, huku watani wao Yanga SC wakiridhika na nafasi ya pili.
Katika orodha ya washindi binafsi, Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, aling’ara kwa kutwaa tuzo ya Kocha Bora wa mashindano, ishara ya kazi kubwa aliyofanya kuifikisha timu hiyo kileleni.
Kiungo chipukizi Hussein Mbegu naye alijizolea tuzo ya Mchezaji Bora Kijana, akionyesha mustakabali mzuri ndani ya kikosi hicho.
Safu ya ulinzi na ushambuliaji nayo haikubaki nyuma, ambapo kipa Hussein Abel alitwaa tuzo ya Kipa Bora wa mashindano, wakati Selemani Mwalimu akiibuka Mfungaji Bora, akihitimisha mashindano kwa ubora mkubwa mbele ya lango.
Licha ya ushindani mkubwa, beki wa Simba, Rushine De Reuck, alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mashindano, akithibitisha ubora wake katika safu ya ulinzi na mchango wake mkubwa kwenye mafanikio ya timu.
Kwa upande wa benchi la ufundi, Steve Barker ameweka alama ya kipekee kwa kutwaa taji lake la kwanza tangu ajiunge na Simba mwanzoni mwa msimu huu, mafanikio yanayoashiria mwanzo mzuri wa safari yake ndani ya klabu hiyo.
Ubingwa huo pia umeifanya Simba kufikia rekodi ya watani wao Yanga, ambapo sasa kila timu imetwaa Kombe la Muungano mara saba, jambo linalozidi kuongeza ushindani mkali kati ya vigogo hao wa soka la Tanzania.