Home Habari za michezo BAO LA MWISHO LAWAVUNJA MOYO MASHABIKI, SIMBA WATAMBA

BAO LA MWISHO LAWAVUNJA MOYO MASHABIKI, SIMBA WATAMBA

0

SIMBA imetwaa ubingwa wa Kombe la Muungano baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Yanga katika fainali iliyopigwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Bao pekee la mchezo huo lilifungwa na Selemani Mwalimu katika dakika ya 120 kwa mkwaju wa penalti, kufuatia Clatous Chama kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari na Edmund John.

Mwamuzi kutoka Kenya, Dickes Mimisa, hakuwa na shaka kuamuru penalti hiyo iliyoamua hatma ya mchezo.

Ushindi huo haukuiwezesha tu Simba kutwaa taji, bali pia kurejesha heshima yao mbele ya wapinzani wao wakubwa Yanga, ambao walikuwa mabingwa watetezi wa michuano hiyo.

Aidha, kwa bao hilo, Mwalimu amefikisha jumla ya mabao matatu katika mashindano hayo, akilingana na mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube, katika orodha ya wafungaji bora.

Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa, dakika 90 za kawaida zilimalizika bila timu yoyote kufanikiwa kutikisa nyavu, hali iliyolazimu kuchezwa kwa dakika 30 za nyongeza kwa mujibu wa kanuni za fainali.

Kipindi cha kwanza kilishuhudia timu zote zikishambuliana kwa zamu, lakini zilikosa umakini wa mwisho wa kufumania nyavu.

Safu za ulinzi za pande zote mbili zilikuwa imara, zikidhibiti hatari zote na kufanya mchezo kubaki mgumu hadi dakika za mwisho.

Hatimaye, penalti ya dakika za lala salama ndiyo iliyobadili mwelekeo wa mchezo na kuipa Simba ubingwa uliosubiriwa kwa hamu kubwa.