Home Habari za michezo SIMBA AWAVURUGA YANGA AKILINI, DABI YA MEI 3 YAWANYIMA USINGIZI

SIMBA AWAVURUGA YANGA AKILINI, DABI YA MEI 3 YAWANYIMA USINGIZI

0

LICHA ya kuwa na kibarua kigumu leo katika fainali ya Kombe la Muungano dhidi ya Simba, Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji, amesema presha ya Kariakoo Derby ijayo tayari imeanza kuwanyima usingizi viongozi na benchi la ufundi.

Arafat amesema uzito wa Derby hiyo unatokana na ushindani mkubwa uliopo kati ya timu hizo mbili, hasa zinapokutana katika Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo kila upande hupambana kulinda heshima yake mbele ya mashabiki.

Ameeleza kuwa baada ya fainali ya leo, Yanga itakuwa na kibarua kingine kigumu Mei 3, 2026, watakapokuwa wageni wa Simba katika mchezo wa Kariakoo Derby utakaochezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni.

Kiongozi huyo amesisitiza kuwa kwa sasa nguvu zote zimeelekezwa kwenye fainali ya Kombe la Muungano, wakilenga kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya Simba na kurejea Dar es Salaam wakiwa mabingwa kabla ya kuanza maandalizi ya mchezo unaofuata.

“Malengo ya Yanga ni kubeba makombe yote tunayoshiriki. Ndio maana viongozi tumekuwa karibu na timu, tukihamasisha wachezaji kuhakikisha wanapambana hadi kutwaa ubingwa wa Kombe la Muungano,” amesema Arafat.

Ameongeza kuwa ratiba ya mechi mbili kubwa mfululizo inaweka shinikizo kubwa kwa timu, kwani baada ya fainali ya leo, watakuwa na siku chache tu za maandalizi kabla ya kukutana tena na Simba.

“Hakuna muda wa kupumzika ndani ya siku hizi tatu kabla ya Derby nyingine. Tunahitaji ushindi. Derby ni mechi ya heshima kubwa, na tangu tumeingia madarakani tumekuwa na matokeo mazuri dhidi ya wapinzani wetu,” amesema.