MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema uongozi wa klabu hiyo unatambua kwa kina changamoto iliyopo katika kikosi, hasa eneo la kiungo, tayari umeanza kuweka mipango ya muda mrefu kuhakikisha pengo la Clatous Chama halibaki wazi pindi muda wake utakapofika mwisho.
Ahmed amesema viongozi wa Simba wameanza mchakato wa mapema wa kusaka wachezaji wenye uwezo wa kurithi majukumu ya nyota huyo raia wa Zambia, ambaye kwa muda mrefu amekuwa mhimili muhimu wa mafanikio ya Wekundu wa Msimbazi ndani ya uwanja.
Ameeleza kuwa Chama si mchezaji wa kawaida ndani ya kikosi hicho, bali ni kiungo tegemeo ambaye mchango wake umebadilisha mwenendo wa Simba katika mechi nyingi muhimu.
Amesema kila anapomtazama uwanjani, hushindwa kujizuia kihisia kutokana na ukubwa wa nafasi yake, huku akitafakari siku ambayo huenda timu italazimika kuendelea bila uwepo wake.
“Kila nikimtazama Chama machozi huwa yananitoka, najiuliza ‘daaah! Mwamba wa Lusaka anamaliza muda wake, tunafanyaje sasa?’ Lakini tunaamini viongozi wetu watatumia muda mwingi kutafuta vijana wengine kuja kurithi mikoba yake, ingawa si jambo rahisi,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa Chama ndiye “turning point” ya mafanikio ya Simba katika miaka ya hivi karibuni, kuwa mchango wake umeifanya timu hiyo kuwa moja ya vikosi hatari zaidi nchini na hata nje ya mipaka ya Tanzania.
Amesema bado nyota huyo yupo kikosini na ataendelea kuitumikia timu kwa nguvu zote, ikiwemo katika mchezo wa fainali ya Kombe la Muungano dhidi ya Yanga.
Ahmed amesisitiza kuwa uongozi wa Simba upo makini na unaendelea kupanga mikakati ya kuhakikisha kikosi kinabaki imara hata baada ya kipindi cha Chama kufika tamati, akibainisha kuwa mchakato wa kupata mbadala wake ni wa muda, utaalamu na uvumilivu mkubwa.
Kauli ya Ahmed inaonyesha ukubwa wa thamani ya Chama ndani ya Simba SC, pia ikifichua changamoto ya kimkakati inayoikabili klabu hiyo katika kuhakikisha inabaki kwenye ushindani wa kiwango cha juu hata baada ya nyota huyo kuhitimisha safari yake Msimbazi.