MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema ushindi walioupata dhidi ya Yanga katika fainali umefuta uteja wa kufungwa mara sita mfululizo na kurejesha imani kwa kikosi hicho.
Amesema matokeo hayo yanaonyesha mabadiliko makubwa ndani ya timu, huku akisisitiza kuwa sasa wapinzani wao watalazimika kuwa na tahadhari kubwa wanapokutana na Simba kutokana na uimara wa kikosi chao.
Ahmed amewakumbusha kuwa hata katika mzunguko wa kwanza waliocheza Zanzibar, Simba walifunga bao ambalo halikukubaliwa na mwamuzi msaidizi na hivyo kulazimika kutoka sare, jambo ambalo linaonyesha kuwa walikuwa na uwezo tangu awali.
“Leo tumewafunga na kutwaa ubingwa, hii inaonyesha wazi namna timu yetu ilivyoimarika na kuwa bora zaidi,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa kutokana na ubora wa kikosi chao kwa sasa, si sahihi kwa wapinzani wao kuingia uwanjani wakiwa na dhana ya kuwafunga kirahisi kama ilivyokuwa awali.
“Kwa sasa tuna uwezo wa kupata matokeo mazuri dhidi yao. Wasikalili matokeo ya nyuma, wanapaswa kuja kwa heshima na tahadhari kubwa,” ameongeza.
Baada ya ushindi huo wa fainali, Simba sasa inaelekeza nguvu zake kwenye mchezo mwingine mgumu wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Yanga, maarufu kama Kariakoo Derby, utakaopigwa Jumapili, Mei 3, 2026 katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni.