BAADA ya kupoteza fainali ya Kombe la Muungano kwa kufungwa bao 1-0 na Simba katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves amesema matokeo hayo ni sehemu ya kujifunza na kuboresha mapungufu kabla ya majukumu yajayo, hususan Kariakoo Derby.
Pedro ameeleza kuwa licha ya kupoteza taji, ameridhishwa na kiwango cha ushindani kilichoonyeshwa na wachezaji wake, akisisitiza kuwa timu ilipambana kwa hali ya juu kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mashindano.
Amebainisha kuwa nidhamu, kujitoa na umoja wa kikosi chake vilijidhihirisha wazi katika michezo yote ya Kombe la Muungano, jambo linalompa imani kubwa ya kufanya vizuri zaidi katika mechi zijazo.
“Tunajivunia timu hii kwa namna ilivyopambana katika Kombe la Muungano. Kujitoa, tabia njema na umoja vimeonekana hadi mwisho kabisa,” amesema Pedro.
Ameongeza kuwa kwa sasa wanahamishia nguvu zao kwenye mchezo ujao wa Jumapili pamoja na mechi za Ligi Kuu Bara, wakilenga kulinda nafasi yao ya juu waliyoipata kwa juhudi zao wenyewe.
Kocha huyo pia amewaomba mashabiki wa Yanga kuendelea kuiunga mkono timu hiyo, akisisitiza kuwa mchango wao ni mkubwa katika kuwapa morali wachezaji na kuisukuma timu kufikia malengo yake.
“Asanteni sana Wananchi kwa sapoti yenu ya kipekee—tunaiona na kuihisi kila hatua ya safari,” ameongeza.
Pedro amesisitiz kuwa Yanga bado inaongoza msimamo wa ligi, hivyo ni wajibu wao kupambana kwa nguvu zote kuhakikisha wanaendelea kubaki kileleni hadi mwisho wa msimu.