Home Habari za michezo KWANINI CHAMA HAKUPIGA PENALTI, MAAMUZI YA SIMBA KUCHUKUA UBINGWA WAZI

KWANINI CHAMA HAKUPIGA PENALTI, MAAMUZI YA SIMBA KUCHUKUA UBINGWA WAZI

0

KIUNGO wa Simba SC, Clatous Chama, amefunguka sababu mbili kuu zilizomfanya aamue kutopiga penalti aliyopata timu yake katika fainali ya Kombe la Muungano na badala yake kumkabidhi jukumu hilo Selemani Mwalimu, hatua iliyozaa matunda muhimu kwa Wekundu wa Msimbazi.

Tukio hilo lilitokea jana katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar, ambapo Simba waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Yanga SC katika mchezo uliokuwa na presha kubwa na ushindani mkali hadi dakika za mwisho.

Bao pekee la mchezo lilipatikana dakika ya 120 kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na Selemani Mwalimu, baada ya Clatous Chama kuangushwa ndani ya eneo la hatari na beki wa Yanga, Edmund John, hali iliyosababisha mwamuzi kutoka Kenya, Dickes Mimisa, kuamuru penalti hiyo ipigwe.

Kabla ya mkwaju huo kupigwa, Chama akiwa na mpira aliwaita viongozi wa karibu uwanjani akiwemo nahodha Shomari Kapombe, ambapo walijadiliana kwa sekunde kadhaa kuhusu mpigaji sahihi wa penalti hiyo ya maamuzi.

Chama amesema sababu ya kwanza iliyopelekea kumpa Mwalimu jukumu hilo ni utaratibu wa timu yao, kwani Selemani Mwalimu ni miongoni mwa wachezaji walioteuliwa rasmi kupiga penalti endapo nafasi hiyo itatokea katika mechi yoyote.

Sababu ya pili, Chama amebainisha  kuwa alitaka Mwalimu apate nafasi ya kuongeza nafasi yake katika orodha ya wafungaji bora wa mashindano, jambo ambalo lilifanikiwa baada ya kufunga bao hilo muhimu lililoipa Simba ubingwa wa Kombe la Muungano, mashindano yaliyofanyika kama sehemu ya kalenda ya mashindano ya Muungano.