Home Habari za michezo BACCA AWATULIZA WANANCHI, SUBIRA, TUTARUDI TUKIWA HATARI

BACCA AWATULIZA WANANCHI, SUBIRA, TUTARUDI TUKIWA HATARI

0

BEKI wa Yanga, Ibrahim Hamad maarufu kama Bacca, amewataka mashabiki wa timu hiyo kubaki wamoja na kuwa na subira kufuatia matokeo ya hivi karibuni yaliyowaumiza wengi.

Bacca amesema anafahamu kuwa hali ya jana imewaumiza mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo, lakini akasisitiza umuhimu wa kuheshimu matokeo na kuendelea kusonga mbele kwa moyo mmoja.

Ameeleza kuwa katika nyakati ngumu kama hizi, kitu kikubwa kinachohitajika ni umoja ndani na nje ya uwanja, huku akiwataka mashabiki kutochukulia matokeo hayo kama mwisho wa safari.

“Tunajua mnapitia mengi kutokana na matokeo ya jana, lakini ni muhimu kuheshimu kilichotokea na kuwa na subira,” amesema Bacca.

Beki huyo ameongeza kuwa wanapaswa kusahau haraka kilichopita na kuelekeza nguvu zao katika mechi zijazo, akiamini kuwa kesho ya Yanga itakuwa bora zaidi iwapo kila mmoja atabaki na imani.

Bacca amewahakikishia mashabiki kuwa kikosi hicho kitaendelea kupambana kwa bidii ili kurejesha furaha yao, akisisitiza kuwa matumaini bado yapo na mustakabali wa timu ni mzuri, Inshaallah.

Yanga ina kibarua kingine kizito Jumapili katika mchezo wa Ligi Kuu ambapo itakutana tena na Simba kwenye Uwanja wa Jenerali Isamuhyo, mchezo wa jasho au damu katika mbio za ubingwa.