Home Habari za michezo BARKER CHINI YA PRESHA, SIMBA WAKITAKA MAKUBWA AFRIKA

BARKER CHINI YA PRESHA, SIMBA WAKITAKA MAKUBWA AFRIKA

0

UONGOZI wa klabu ya Simba umempa kazi nzito kocha wake, Steve Barker, baada ya kuweka wazi kuwa bado hawajaridhishwa na kiwango cha kikosi hicho kulingana na malengo makubwa ya klabu.

Kauli hiyo imekuja licha ya Barker kufanikisha Simba kutwaa ubingwa wa Kombe la Muungano, kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya watani wao Yanga katika fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Mwenyeki wa Bodi ya Wakurugenzi Simba,  Crescentius Magori amesema ushindi huo haukuwa rahisi kutokana na ugumu wa mechi iliyodumu kwa dakika 120, hali iliyowaacha wachezaji wakiwa wamechoka kuelekea mechi nyingine muhimu inayofuata.

“Mechi ilikuwa ngumu sana, dakika 120 za jasho na damu. Bado tuna siku mbili au tatu kabla ya kucheza mechi nyingine ngumu, hivyo wachezaji wanapaswa kupona haraka na kujiandaa kwa mchezo wa Jumapili,” amesema.

Magori ameweka  wazi kuwa ushindi huo hauondoi ukweli kwamba bado kiwango cha timu hakijafikia matarajio ya uongozi, akisisitiza kuwa Simba inalenga zaidi mafanikio ya kimataifa kuliko ya ndani pekee.

“Bado sijaridhishwa na kile nilichokiona. Timu yetu inapaswa kucheza zaidi ya hapa tulipo kwa sababu tunajenga kikosi si kwa ajili ya Ligi ya Tanzania tu, bali kwa ushindani wa Afrika. Hii timu bado inajengwa,” ameongeza.