Home Habari za michezo RONALDO AZUNGUMZA KWA MARA YA KWANZA ISHU YA KUSTAAFU

RONALDO AZUNGUMZA KWA MARA YA KWANZA ISHU YA KUSTAAFU

0

RIYADH, SAUDI ARABIA: GWIJI wa soka duniani, Cristiano Ronaldo, amekiri kwa mara ya kwanza kuwa mwisho wa safari yake ya soka umeanza kukaribia, huku akisisitiza kuwa bado anafurahia kila dakika anayocheza uwanjani.

Ronaldo (41), ambaye anaendelea kupambana na umri wake, amesema kuwa kinachomfanya aendelee kucheza ni mapenzi makubwa aliyonayo kwa mchezo huo baada ya kudumu kileleni kwa zaidi ya miongo miwili.

Akizungumza na CanalGoatBr baada ya kuisaidia Al Nassr kuifunga Al Ahli na kukaribia ubingwa wa Ligi Kuu ya Saudi Arabia, Ronaldo amesema motisha yake inatoka kwa vizazi vyote vya mashabiki.

Licha ya kuendelea kufunga mabao na kuonyesha kiwango cha juu, mshindi huyo mara tano wa tuzo ya Ballon d’Or ameweka wazi kuwa anajua saa ya kuachana na soka inakaribia.

“Naendelea kucheza si kwa ajili ya kizazi hiki pekee, bali pia kwa ajili ya kizazi kilichopita na kile kijacho. Nafurahia siku baada ya siku, mchezo baada ya mchezo, na mwaka baada ya mwaka, hata ninapokaribia mwisho wa kazi yangu. Huo ndio ukweli,” amesema Ronaldo.

Ronaldo, ambaye amepita katika klabu kubwa duniani kama Sporting Lisbon, Manchester United, Real Madrid na Juventus, ameitaja safari yake ya soka imekuwa ya kipekee na anataka kuimaliza kwa kiwango hicho hicho.

“Kazi yangu imekuwa ya kipekee na nataka iendelee kuwa hivyo. Bado nafurahia, naendelea kufunga mabao… lakini zaidi ya yote, ni kuhusu kushinda. Na tunataka sana kushinda ligi msimu huu,” amesema.

Akiwa na umri wa miaka 41, Ronaldo amegoma kushuka kiwango, akiongoza safu ya ushambuliaji ya Al Nassr na timu ya taifa ya Ureno kwa ufanisi mkubwa.

Kauli yake imewacha mashabiki wakijiuliza ni lini hasa atatundika daruga, huku wengi wakitumai kumuona akicheza hadi fainali za Kombe la Dunia 2026.