DIOMANDE, BOUADDI WALIOANZA MAPEMA SANA
IKIWA Ayyoub Bouaddi na Yan Diomande ni dalili ya kitu chochote, basi mustakabali unaonekana kuwa mzuri kwa Morocco na Ivory Coast mtawalia baada ya kuwa na ‘maonyesho’ ya kuvutia katika mechi zao za kwanza za Kombe la Dunia 2026.
Takriban nusu au zaidi kidogo nusu ya mechi za raundi ya kwanza zimeshachezwa, lakini tayari inawezekana umeona vipaji viwili bora vilivyombuliwa katika mashindano hayo.
Bouaddi na Diomande hawakuwa wageni kabisa kabla ya mashindano; kwani Diomande amemaliza msimu akiwa miongoni mwa wachezaji bora zaidi katika Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga), huku Bouaddi akiwa mchezaji wa kikosi cha kwanza wa Lille katika Ligi Kuu Ufaransa (Ligue 1) kwa zaidi ya miaka miwili.
Lakini, katika picha kubwa zaidi, wote wawili walifanya vizuri na kwa njia hiyo wamejitambulisha upya tena katika mashindano yanayoendelea huko Amerika Kaskazini. Bouaddi, 18, alitoa shoo ya ukomavu katikati ya kiungo cha Morocco kwenye sare ya bao 1-1 dhidi ya Brazil, na usiku uliofuata Diomande, 19, aling’ara katika ushindi wa Ivory Coast wa bao 1-0 dhidi ya Ecuador.
iomande alipata mapokezi makubwa zaidi kabla ya mashindano. Hii haimaanishi kupunguza thamani ya Bouaddi, kwa sababu wote wawili walitabiriwa kuwa wachezaji wa kuangaliwa, lakini winga huyo wa Ivory Coast alikuwa akihusishwa sana na Liverpool majira ya joto, na amekuwa mmoja wa wachezaji wanaozungumziwa zaidi Ulaya kuhusiana na uhamisho tangu msimu wa ligi ulipomalizika.
Nyota huyo alionyesha kiwango kilichotarajiwa wakati Ivory Coast ilipoanza kampeni kwa ushindi ambao kwa uwezekano mkubwa utawapeleka hatua ya 32 bora, kwa kuwa wako kwenye kundi moja na Curacao ambao hawatarajiwi kufanya makubwa.
Diomande alichukua muda kuingia mchezoni na jaribio lake la kwanza la kuwavaa mabeki wa Ecuador liliisha kupokonywa mpira dakika ya nane; muda mfupi baadaye alibanwa na Piero Hincapie wa Ecuador aliyempokonya mpira.
Lakini ushawishi wake uliongezeka. Pasi nzuri kwa Seko Fofana pembeni ya eneo la hatari ilimpatia nafasi ya kupiga shuti, lililozuiwa. Kisha akamuandalia Elye Wahi nafasi kwa pasi ya ubunifu nyuma ya safu ya ulinzi, lakini shuti likakosa makali. Baada ya hapo Diomande alizidi kuwa tishio kubwa kwa Hincapie. Kupindua bega na kuongeza kasi ghafla kulimwacha beki huyo wa Arsenal akishindwa kumdhibiti mara kadhaa. Harakati zake za ghafla na mabadiliko ya mwelekeo zilifanya safu ya ulinzi ya Ecuador kuwa na wakati mgumu, matukio yaliyosababisha mipira hatari ndani ya boksi, ingawa hakukuwa na mabao.
Mwisho wa mchezo, alitengeneza nafasi tano za mashambulizi, idadi kubwa zaidi kwenye mashindano hadi sasa; majaribio yake saba ya chenga yakimfanya kuwa miongoni mwa bora. Pia alikuwa juu katika ukokota mpira na kuanzisha mashambulizi hatari. Diomande hakuwa peke yake aliyemtesa Hincapie, kwani Amad Diallo pia alimfanya acheze chini ya presha katika kipindi cha pili. Hata hivyo, kasi na nguvu ya Diomande haitasahaulika kirahisi.
Kwa upande mwingine, Bouaddi aling’ara kwa mtindo tofauti kabisa. Akiwa amebadili uamuzi wake wa kimataifa hivi karibuni kutoka Ufaransa, Bouaddi alipewa nafasi ya kuanza katikati ya kiungo dhidi ya Brazil kwenye uamuzi uliowashangaza wengi kutokana na umri na ukubwa wa mchezo.
Kocha wake, Mohamed Ouahbi, alisema hakushangazwa naye akisema: “Hakunishangaza kwa sababu nilijua tayari yeye ni mchezaji wa aina gani.” Wengi walimuona kiungo wa ulinzi aliyedhibiti mchezo dhidi ya mabingwa mara tano wa dunia na wachezaji pekee waliogusa mpira mara nyingi zaidi kuliko yeye walikuwa mabeki wa kati wa Brazil.
Bouaddi alishuka chini kupokea mpira, akionekana mtulivu hata alipobanwa. Alikamilisha pasi 60 kati ya 66 (asilimia 90.7), na kuwa miongoni mwa wachezaji wachanga zaidi waliokamilisha pasi 50+ katika Kombe la Dunia tangu 1966. Pia alijiamini akiwa na mpira na bila mpira kwa kurejesha umiliki mara sita. Ilikuwa mechi ya ukomavu dhidi ya Brazil na huwezi kupata bora zaidi kuliko hapo kwa mchezo wa kwanza wa Kombe la Dunia. Kila Kombe la Dunia lina nyota wapya wanaochipukia; Bouaddi na Diomande tayari wamejitokeza mapema kama watakaotikisa wakubwa mapema.