Habari za michezo

LEO NI ZAMU YA RONALDO KOMBE LA DUNIA

Vardo June 17, 2026 3:41 pm

HOUSTON, MAREKANI: Kila kizazi huwa na shujaa wake, lakini wachache wameweza kuandika historia inayodumu kwa zaidi ya miongo miwili kama alivyofanya Cristiano Ronaldo ambaye leo atakuwa jijini Houston, Marekani akiwa na Ureno kuanza safari yake ya sita ya Kombe la Dunia dhidi ya DR Congo.

Akiwa na umri wa miaka 41, Ronaldo anaingia kwenye mashindano haya akiwa mchezaji wa pili mwenye umri mkubwa zaidi katika historia ya Kombe la Dunia, nyuma ya gwiji wa Cameroon, Roger Milla.

Lakini tofauti na mastaa wengi wanaofika kwenye michuano mikubwa kwa ajili ya heshima ya mwisho, Ronaldo bado ni silaha muhimu ya Ureno.

Tangu kocha Roberto Martinez achukue timu hiyo mwaka 2023, mshambuliaji huyo amecheza mechi 26 na kufunga mabao 22, takwimu zinazoonyesha bado ana uwezo wa kuamua matokeo ya mechi kubwa.

NDOTO ILIYOSALIA

Katika kabati lake la mataji, Ronaldo ana karibu kila kitu. Amebeba mataji ya ligi mbalimbali, ameshinda mara tano tuzo ya Ballon d’Or, ameshinda UEFA European Championship 2016 na pia UEFA Nations League.

Lakini kuna kitu kimoja kinachokosekana, ambacho ni Kombe la Dunia. Mafanikio yake makubwa katika michuano hiyo yalikuwa mwaka 2006 alipofika nusu fainali. Tangu hapo ameshuhudia maumivu ya kutolewa hatua ya makundi mara mbili, hatua ya 16 bora na robo fainali.

Ndiyo maana safari hii ya 2026 inaonekana kuwa muhimu zaidi katika maisha yake ya soka.

URENO YENYE NJAA YA MAFANIKIO

Ureno inaingia kwenye mashindano hayo ikiwa katika nafasi ya tano kwenye viwango vya FIFA na ikiwa na kikosi chenye mchanganyiko wa uzoefu na vipaji.

Pembeni mwa Ronaldo wapo viungo wabunifu kama Bruno Fernandes na Bernardo Silva. Katika miaka miwili iliyopita, Ureno imeonyesha kurudi kwenye hadhi ya mataifa makubwa baada ya kutwaa UEFA Nations League na kufanya vizuri katika michuano ya Ulaya.

DR CONGO SI WAKUPUUZWA

Ingawa Ureno ndiyo inapewa nafasi kubwa ya kushinda, wapinzani wao hawataki kuwa wasindikizaji.

DR Congo imerejea Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1974 iliposhiriki kwa jina la Zaire.

Kikosi hicho kinaongozwa na mshambuliaji hatari Yoane Wissa pamoja na mkongwe Cédric Bakambu, huku nguvu kubwa ikionekana pembeni kupitia Aaron Wan-Bissaka na Arthur Masuaku.

Hata hivyo, uzoefu wa Ronaldo na ubora wa kikosi cha Ureno vinaifanya mechi hii ionekane kama fursa kwa gwiji huyo.

HISTORIA INASUBIRI

Iwapo Ronaldo atafunga katika mashindano haya, ataendelea kupanua rekodi zake ambazo tayari zimemfanya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa soka la kimataifa akiwa na mabao 138.

Lakini zaidi ya mabao, macho ya mashabiki duniani yatakuwa yakitafuta kuona kama safari hii ndiyo itakayompa kile alichokikosa kwa miaka zaidi ya 20: kuinua Kombe la Dunia.

Huenda huu ukawa mwisho wa simulizi ya mmoja wa wachezaji wakubwa zaidi kuwahi kutokea duniani. Na kama ilivyo kwa hadithi zote kubwa, Ronaldo anataka sura ya mwisho iandikwe kwa herufi za dhahabu.

USAJILI WA GIRUMUGISHA YANGA, KAMWE AWEKA MAMBO WAZI DIOMANDE, BOUADDI WALIOANZA MAPEMA SANA