Home Habari za michezo HAKUNA ANAYETAKA KUKUTANA NA SIMBA YA BARKER

HAKUNA ANAYETAKA KUKUTANA NA SIMBA YA BARKER

0

KOCHA Mkuu wa Simba, Steve Barker, ameendelea kuwa gumzo miongoni mwa wadau wa soka kufuatia mabadiliko makubwa yaliyoonekana ndani ya kikosi hicho katika kipindi kifupi tangu ajiunge na timu hiyo.

Kwa mujibu wa Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, ndani ya miezi michache tu kocha huyo ameibadilisha timu na kuifanya ionekane tishio kwa wapinzani wake, jambo lililozua mjadala mpana kuhusu ubora wake katika msimu huu.

Kauli za sifa zimekuwa zikitolewa kutoka pande mbalimbali, huku wengi wakiamini Barker anastahili kutajwa miongoni mwa makocha bora kwa sasa kutokana na mchango wake mkubwa ndani ya muda mfupi.

Ahmed ameenda mbali zaidi akisisitiza kuwa hahitaji kusubiri hadi mwisho wa msimu kuthibitisha uwezo wa kocha huyo, kwani alichokifanya tayari kinajidhihirisha wazi uwanjani.

“Katika muda mfupi aliokaa na timu, ameibadilisha Simba kiuchezaji na kisaikolojia. Wachezaji wana ari mpya, nidhamu ya hali ya juu, pamoja na mbinu zinazowafanya wapinzani washindwe kuisoma timu kirahisi,” amesema Ahmed.

Ameongeza kuwa Simba imeanza kuogopwa tena kama ilivyokuwa zamani, huku akikumbusha pia mafanikio ya Barker katika timu nyingine, ambapo aliwahi kufanikisha makubwa licha ya kuwa na kikosi kisichopewa nafasi kubwa.

“Haijalishi mwisho wa msimu utakuwaje, lakini ni wazi Steven Barker ni kocha bora kwa sasa. Ni ‘game changer’ wa kweli; ndani ya miezi minne tu ameifanya Simba kuwa tishio, na sasa hakuna timu inayotamani kukutana nasi,” ameongeza.

Ahmed pia alibainisha kuwa haishangazi kuona kocha huyo aliwahi kuifikisha Stellenbosch hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho, licha ya kuwa timu hiyo haikuwa ikipewa nafasi kubwa.
“Asante Mwana Mapinduzi, Barker amebakiza hatua chache tu kurejesha makali yetu si ndani pekee bali hata Afrika. Katika mechi tatu za dabi, ameshinda mbili na kutoka sare moja,” amesema Ahmed.