KOCHA Mkuu wa Mlandege, Hassan Ramadhan ‘Pele’ amesema ushindi walioupata dhidi ya Zimamoto umefufua matumaini mapya ya timu hiyo kutetea taji lao la Ligi Kuu Zanzibar.
Katika mchezo huo uliopigwa Mei 2, 2026 kwenye Uwanja wa Mao A kisiwani Unguja, Mlandege iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Zimamoto.
Ushindi huo umeifanya Mlandege kupanda hadi nafasi ya tano katika msimamo wa ligi hiyo ikifisha pointi 40 sawa na ilizonazo Zimamoto iliyoshuka nafasi moja na kuwa ya sita baada ya kupoteza mchezo huo.
Kocha Pele amesema dhamira yao ilikuwa ni kuondoka na alama tatu ambazo zitawasaidia kupambana kutetea ubingwa wao au kumaliza ndani ya nne bora jambo ambalo wamefanikiwa.
Amesema, kwa sasa wamebakisha michezo sita na malengo yao ni kushinda yote ili msimu ujao wapate nafasi ya kushiriki tena mashindano mbalimbali ikiwemo kimataifa.
“Bado timu yetu inahitaji kuiwakilisha Zanzibar kwenye mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa, hivyo tukikosa kutetea taji letu tunahitaji tuchukue ubingwa wa FA ili tushiriki mashindano ya kimataifa,” amesema Pele.
Kituo kinachofuata sasa ni Derby ya Mjini kati ya Mlandege dhidi ya Malindi ambapo katika mzunguko wa kwanza Mlandege iliibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Kwa mzunguko huu, hii itakuwa zaidi ya dabi kwa sababu Mlandege inapambana kumaliza nafasi nne za juu, huku Malindi ikijipapatua isishuke daraja.