Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi, ameiomba Serikali kumpa uraia wa heshima kiungo wa Simba SC, Clatous Chama akitaja mambo matatu.
Shangazi ametoa kauli hiyo Bungeni leo Jumatatu Mei 4, 2026 ambapo ameyataja mambo hayo ni bao zuri alilofunga kiungo huyo kwenye Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga iliyochezwa jana Jumapili, kuwa na uwezo wa kuzungumza Kiswahili na namna ambavyo ameisaidia Simba kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mchango wake kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Shangazi amesema kuwa mchezaji pekee ambaye alipaswa kupewa uraia wa Tanzania ni Chama kwani anazo sifa za namna hiyo.
“Yeye ana mambo matatu, kwanza alifunga goli zuri huenda kuliko magoli yote, pili anazungumza Kiswahili vizuri lakini tatu kwa kutumia miguu yake ameshaipeleka Simba mara mbili robo fainali ya mashindano ya Afrika, nadhani angepewa uraia huyu siyo wale wengine,” amesema Shangazi.
Hata hivyo, Mbunge wa Geita Vijiji, Joseph Musuka ameomba kumpa taarifa shangazi akimtaka atambue kuwa bao alilolifunga Chama dhidi ya watani wao Yanga, alikuwa ameotea ingawa mwamuzi hakuona hilo, kauli iliyokataliwa na Shangazi.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Revocatus Chipando maarufu Baba Levo, amemuomba Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda kuruhusu wabunge watafute vijana wenye vipaji kutoka majimboni ndiyo waunde timu ya taifa.
Baba Levo amesema kuwa ni aibu Taifa kupeleka wachezaji wazee na kwamba itachangia kupokea kipigo kama cha ng’ombe.
“Wale wazee akili inataka lakini mwili unagoma, mheshimiwa Waziri wale hawaji kuangalia kama sisi ndiyo wenyeji wa mashindano eti watuonee huruma, tutapokea kipigo kama ng’ombe, mtakuja kuniambia,” amesema Baba Levo.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo, kwa sasa wachezaji wengi umri wao umesogea, hivyo hawawezi kutoa matokeo tarajiwa kuelekea ushiriki wa AFCON 2027 ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.