KOCHA Mkuu wa Mbeya City, Salum Mayanga, amesema timu yake haihitaji maneno mengi bali inapaswa kupambana kwa nguvu uwanjani ili kujinasua na hatari ya kushuka daraja.
Mbeya City kwa sasa inashika nafasi ya 13 kwenye msimamo ikiwa na alama 21 baada ya kucheza michezo 21, huku ikiwa bado na mechi tisa mkononi ambazo zinahitaji matokeo mazuri ili kujihakikishia usalama.
Mayanga amesisitiza kuwa kikosi chake kinaendelea kupambana katika kila mchezo kwa lengo la kusaka ushindi, akiamini kuwa wana uwezo wa kufanya vizuri katika michezo iliyosalia.
Ameeleza kuwa bado anaifanyia kazi safu ya ulinzi ambayo imekuwa na changamoto katika baadhi ya mechi zilizopita.
Hata hivyo, katika mchezo wa jana dhidi ya Tanzania Prisons, licha ya kuruhusu bao, walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 ndani ya dakika 90 za Ligi Kuu.
“Mpira ni mchezo wa makosa, hivyo kuna mambo tunaendelea kuyarekebisha. Tunafanya kazi na wachezaji kuhakikisha hatuyarudii makosa yale yale,” amesema Mayanga.
Kocha huyo ameongeza kuwa tayari wameanza safari kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao ujao wa ugenini dhidi ya JKT Tanzania utakaochezwa Mei 9, 2026.
Amesema wanatarajia kukutana na timu imara iliyo katika nafasi ya nne kwenye msimamo, lakini wamejipanga kupambana ili kupata matokeo chanya yatakayowasaidia kujiweka katika nafasi nzuri na kuendelea kubaki salama kwenye ligi.