MSIMBAZI WAMUWINDA MSHAMBULIAJI ALIYETIKISA AFRIKA
UONGOZI wa Simba unaendelea na harakati za kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao, huku ukiweka nguvu kubwa katika kusaka mshambuliaji mwenye uwezo wa kufunga mabao kwa kiwango cha juu katika michuano ya ndani na kimataifa.
Taarifa zinaeleza kuwa mabosi wa klabu hiyo kwa sasa wako kwenye mazungumzo na mshambuliaji wa Stade Malien ya Mali, Taddeus Nkeng, raia wa Cameroon, ambaye ameonyesha kiwango bora katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu ujao.
Inaelezwa kuwa Nkeng, bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Stade Malien, jambo linaloifanya Simba kuingia katika mchakato wa kujadiliana namna ya kuvunja mkataba huo ili iweze kupata saini yake mapema kabla ya kuanza kwa msimu mpya.
Mshambuliaji huyo alijizolea sifa nyingi msimu uliopita baada ya kufunga mabao manne katika mechi tano za CAF, rekodi iliyomuweka kwenye rada za klabu kadhaa zinazohitaji kuimarisha safu zao za ushambuliaji.
Ndani ya Simba, maboresho ya eneo la ushambuliaji yamepewa kipaumbele maalumu baada ya benchi la ufundi kubaini umuhimu wa kuwa na washambuliaji wenye uwezo wa kutumia vizuri nafasi za kufunga mabao katika mechi kubwa.
Chanzo cha karibu na klabu hiyo kimeeleza kuwa viongozi wa Simba wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanampata Nkeng, wakiamini anaweza kuongeza ushindani mkubwa katika safu ya ushambuliaji na kuisaidia timu kufikia malengo yake ya msimu ujao.
Iwapo mazungumzo hayo yatakamilika kwa mafanikio, Nkeng ataungana na nyota wengine wanaotarajiwa kujiunga na Simba katika dirisha hili la usajili, hatua ambayo itaongeza nguvu ya kikosi hicho katika mbio za kutwaa mataji ya ndani na kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya CAF.