BAADA YA AZAM, MOALIN AIGEUKIA TRA UNITED KWA UMAKINI MKUBWA
KOCHA Mkuu wa Yanga, Abdulhamid Moalin, amesema bado timu yake haijamaliza kazi katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara licha ya kupata ushindi muhimu dhidi ya Azam FC.
Moalin alisema ushindi huo umeongeza matumaini ya kutwaa taji la ligi, lakini si wakati wa kushangilia kwani bado kuna mechi mbili ngumu zilizobaki ambazo zitakuwa na mchango mkubwa katika kufikia malengo ya msimu.
Kocha huyo amesisitiza kuwa Yanga inapaswa kuendelea kuwa makini na kupambana kwa nguvu zote hadi mwisho wa msimu, akiamini wapinzani waliobaki wana uwezo wa kutoa ushindani mkubwa.
Yanga inatarajiwa kushuka dimbani Juni 27, 2026 dhidi ya TRA United katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam, kabla ya kuhitimisha msimu kwa mechi ya ugenini dhidi ya JKT Tanzania.
Moalin amesema michezo hiyo miwili si rahisi kutokana na namna timu hizo zilivyowapa wakati mgumu katika mzunguko wa kwanza, jambo linalowalazimu kuingia uwanjani kwa tahadhari kubwa.
“Ni mechi ngumu zilizobaki na timu zote mbili zilitusumbua katika mzunguko wa kwanza. Bado hatujauchukua ubingwa hadi tushinde mechi zetu mbili zilizobaki ili kufikia malengo yetu,” amesema Moalin.
Ameongeza kuwa baada ya kumalizana na Azam FC, sasa akili na nguvu zote zimehamia kwenye maandalizi ya mchezo dhidi ya TRA United.
Ingawa muda wa kujiandaa ni mfupi, alisema Yanga italazimika kupambana kwa kila hali kuhakikisha inakusanya alama tatu muhimu zitakazoiweka karibu zaidi na kutimiza ndoto ya kutwaa ubingwa.