TAHADHARI YATOLEWA SIMBA, SINGIDA SIO TIMU YA KUBEZA
KUELEKEA hatua za mwisho za msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba imeanza maandalizi makubwa kuelekea mchezo wake muhimu dhidi ya Singida Black Stars, mechi inayotarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi kutokana na ushindani wa timu hizo.
Wekundu wa Msimbazi wanatambua kuwa hawatakutana na mpinzani wa kawaida, jambo lililomfanya Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, kuwataka wachezaji kuwa makini huku akisisitiza umuhimu wa maandalizi ya kina ili kuhakikisha wanapata matokeo chanya.
Simba inatarajiwa kuwakaribisha Singida Black Stars Jumamosi, Juni 27, 2026, kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, katika mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Akizungumza kuelekea pambano hilo, Ahmed amesema kila mmoja ndani ya kikosi anatambua ubora wa Singida Black Stars na changamoto inayowasubiri, hivyo hakuna nafasi ya kubeza mchezo huo.
“Tunakwenda kucheza mechi ngumu sana dhidi ya Singida. Kila mmoja anajua ni timu ya aina gani, hivyo unapoenda kucheza nao unajua kabisa unakwenda kukutana na mpinzani mwenye uwezo mkubwa. Tunafahamu ubora wao na namna wanavyocheza, kwa hiyo ni mchezo mgumu kweli katika kipindi hiki cha msimu,” amesema Ahmed.
Pamoja na ugumu wa mchezo huo, Ahmed amesisitiza kuwa Simba haina budi kuendelea kupambana kwa nguvu zote, huku lengo likiwa ni kuondoka na alama tatu muhimu zitakazowasaidia katika harakati zao za kutimiza malengo ya msimu.
Ameeleza kuwa benchi la ufundi pamoja na wachezaji wanaendelea na maandalizi maalumu wakitambua uzito wa mchezo huo, hasa katika kipindi hiki ambacho kila pointi ina thamani kubwa.
Kwa mujibu wa Ahmed, kikosi hicho tayari kimerejea kambini baada ya mchezo wake uliopita na kuanza rasmi maandalizi ya kuikabili Singida Black Stars.
Leo timu hiyo imeendelea na mazoezi chini ya Kocha Mkuu, Steve Barker, huku ikinoa makali na kuweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inatumia vyema faida ya kucheza nyumbani kwa lengo la kuvuna pointi zote tatu na kuendelea kuwa kwenye mstari wa kutimiza malengo yake msimu huu.