LICHA ya kutoka sare mara mbili kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na kuibuka na ushindi katika fainali ya Kombe la Muungano, Simba bado inaonyesha dhamira ya kutaka kukutana na Yanga katika fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB.
Katika michuano hiyo, Simba itakutana na TRA United kwenye hatua ya robo fainali, ambapo mshindi wa mchezo huo atatinga nusu fainali na kuvaana na mshindi kati ya Singida BS na Kagera Sugar.
Hii inaipa Simba nafasi ya kuendelea kusaka tiketi ya kufika hatua ya mwisho iwapo itaendeleza ubora wake uwanjani.
Kwa upande wa Yanga, wao watakabiliana na Stand United katika robo fainali, huku mshindi wa pambano hilo akitarajiwa kukutana na mshindi kati ya JKT Tanzania na Pamba Jiji FC katika hatua ya nusu fainali.
Pamoja na mpangilio huo wa michezo, Simba inaonekana kuwa na kiu ya kukutana tena na watani wao wa jadi Yanga, safari hii ikiwa ni kwenye fainali, baada ya kuanza kufuta uteja uliokuwa ukiwasumbua kwa muda mrefu.
Akizungumza kwa niaba ya klabu, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kikosi cha sasa kimeleta mabadiliko makubwa, kikiondoa hali ya unyonge na kurejesha heshima pamoja na hadhi ya timu hiyo.
Amesisitiza kuwa matokeo ya hivi karibuni, yakiwemo sare dhidi ya Yanga na ushindi katika fainali ya Kombe la Muungano, yanaonyesha mwelekeo mzuri wa mafanikio, huku wakilenga kuendelea kuboresha kikosi ili kuwa tishio zaidi msimu ujao.
“Tumetoka kwenye kipindi cha kupoteza mfululizo, sasa wapinzani wanaona fahari kupata sare dhidi yetu, hii inaonyesha tumepiga hatua kubwa, tumeondoa uteja, kilichobaki ni kusimika utawala wetu rasmi. Kwa sasa Yanga hawana uwezo wa kutufunga, kinachobaki ni sisi kuendelea kuwafunga,” amesema Ahmed.