Home Habari za michezo TULIWAPA YANGA UHAI KWA MAKOSA YETU, TULISTAHILI KUWAUWA, BARKER

TULIWAPA YANGA UHAI KWA MAKOSA YETU, TULISTAHILI KUWAUWA, BARKER

0

KOCHA Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amefunguka kuhusu sababu iliyopelekea timu yake kutoka sare ya 2-2 na Yanga SC katika Kariakoo Derby iliyochezwa jana katika dimba la Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni.

Barker amesema licha ya Simba kuonyesha mpira bora hasa kipindi cha kwanza, makosa ya kiufundi na ya kimkakati yaliwapa Yanga nafasi ya kurudi mchezoni na kusawazisha.

“Tulianzia vizuri sana, tulipata mabao mawili mapema na tukatawala mchezo, Hapo ndipo tulipoonyesha ubora wetu,” amesema kocha huyo.

Kwa mujibu wa Barker, Simba walistahili kuibuka na ushindi kutokana na namna ilivyodhibiti mchezo katika dakika za mwanzo. Hata hivyo amekiri kuwa baada ya kuongoza 2-0, wachezaji walipoteza umakini na kufanya makosa yaliyogharimu.

“Tulijua Yanga ni timu kubwa, ukifanya makosa mbele yao wanaadhibu, tulipoteza umakini na tukasawazishiwa mabao yote mawili,” amesema.

Licha ya kuumizwa na matokeo hayo, Barker amesema timu imewasha moto wa kusahau kilichopita na kurejea kwenye uwanja wa mazoezi.

Lengo sasa ni kusahihisha makosa na kujiandaa kwa mechi zijazo za Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la CRDB.

Kocha huyo anaamini kuwa Simba bado ina kila kitu cha kupambana nalo msimu huu, iwapo wachezaji watajifunza kutokana na makosa ya jana na kuweka umakini kwa dakika 90 zote.