Home Habari za michezo SIMBA YAPIGA HESABU MPYA UBINGWA, AHMED ATOA KAULI KALI

SIMBA YAPIGA HESABU MPYA UBINGWA, AHMED ATOA KAULI KALI

0

MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, ameibua matumaini mapya kwa mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi baada ya kusisitiza kuwa mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara bado hazijafungwa, licha ya timu yao kuwa nyuma kwa pointi tano dhidi ya vinara Yanga.

Akizungumza kuhusu hali ya ushindani wa ligi, Ahmed amesema Simba haijakata tamaa na bado inaamini kuwa kila kitu kinawezekana kutokana na mechi zilizobaki. “Sisi tunaamini ubingwa upo wazi, zimesalia mechi 10 ni marufuku kukata tamaa,” amesema.

Ameongeza kuwa katika soka lolote linaweza kutokea, hasa pale ambapo msimu unafikia hatua za mwisho na kila timu inapambana kuhakikisha inapata matokeo chanya. Kwa upande wao, Simba imejipanga kutumia kila nafasi iliyobaki kuhakikisha inakusanya pointi muhimu.
Ahmed amebainisha kuwa wachezaji wa Simba wanaelewa uzito wa nafasi waliyonayo na wamejipanga kupambana katika kila mchezo hadi dakika ya mwisho ya msimu ili kufanikisha malengo yao ya kutwaa ubingwa.

Kauli hiyo inakuja wakati Simba ikijiandaa na mchezo mwingine muhimu dhidi ya JKT Tanzania, ambapo wanahitaji ushindi ili kuendelea kuwasogelea vinara Yanga na kuweka presha katika mbio hizo za ubingwa.

Kwa ujumla, Simba imeweka mkakati wa kushinda mechi zilizosalia zote huku ikisubiri matokeo ya wapinzani wao, wakiamini bado kuna nafasi ya kubadilisha hali ya msimamo wa ligi kabla ya msimu kufikia tamati.