Nahodha wa Yanga SC, Bakari Mwamnyeto, amesema bao alilofunga na kuisaidia timu yake kusawazisha dhidi ya Simba SC ndilo bora zaidi katika maisha yake ya soka, akilitaja pia kuwa la kwanza kwake kufunga katika mchezo wa dabi ya Kariakoo.
Mchezo huo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa Jumapili iliyopita katika hali ya ushindani mkubwa, ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2, baada ya Yanga kurejea mara mbili nyuma na kusawazisha matokeo.
Akizungumzia bao hilo, Mwamnyeto amesema hakuwahi kutarajia kama angeweza kuingia kwenye orodha ya wafungaji katika mchezo huo mkubwa, lakini juhudi binafsi, mshikamano wa kikosi na maelekezo ya benchi la ufundi yalichangia mafanikio hayo.
Beki huyo wa kati amekiri kuwa mchezo huo haukuwa rahisi hata kidogo, akieleza namna walivyokutana na presha kubwa baada ya kuruhusu mabao, jambo lililowalazimu kuongeza umakini na kupambana hadi mwisho.
Ameongeza kuwa akiwa kama nahodha, alijitahidi kuwatia moyo wenzake ndani ya uwanja, hasa wale ambao hawakuwa na uzoefu wa kucheza dabi, ambao mwanzoni walionekana kuyumba kutokana na presha ya mchezo huo mkubwa.
βKocha alituambia tusikate tamaa, kila kitu kinawezekana katika soka. Tulipata maelekezo tukayaweka vizuri na hatimaye tukarudi kwenye mchezo na kufanikiwa kusawazisha,β amesema Mwamnyeto.