USHINDI ndio kauli kuu ya Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Gonçalves, kuelekea mchezo wa kesho wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC FC utakaopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge.
Kocha huyo amesema kikosi chake kimejipanga kuhakikisha kinaendelea na mwendo wake wa ushindi katika ligi.
Pedro ameweka wazi kuwa lengo kubwa la Yanga ni kushinda kila mchezo bila kujali jina la mpinzani.
Amesisitiza kuwa kila mechi kwa sasa ni fainali, hivyo wanatakiwa kuingia uwanjani wakiwa na umakini wa hali ya juu ili kutimiza malengo yao ya ubingwa.
Akizungumzia wapinzani wao KMC FC, Pedro amesema anaifahamu hali yao kwenye msimamo wa ligi ambapo wanashika mkia wakiwa na alama tisa pekee, lakini hilo halimaanishi kuwa ni mechi rahisi.
Amesema KMC wataingia uwanjani kwa morali kubwa wakihitaji alama muhimu kujinusuru.
“Bado wana malengo yao kwenye ligi, watapambana vikali kutafuta matokeo. Wataingia uwanjani kwa kutuheshimu kwa sababu wanakutana na timu inayoongoza ligi,” amesema Pedro.
Ameongeza kuwa Yanga haijali inacheza na nani, bali lengo lao ni moja tu kuchukua alama tatu kila mchezo.
Amesema wachezaji wake wameelewa vizuri falsafa hiyo ya kutodharau mpinzani yeyote, iwe mkubwa au mdogo.
Katika maandalizi ya mchezo huo, Pedro amesema timu ilipata mapumziko baada ya wiki mbili za kambi, na sasa imeanza tena mazoezi ya mwisho.
Ameeleza kuwa anaamini maandalizi ya mwisho yatawasaidia kupata matokeo mazuri na kuhakikisha wanaondoka na alama tatu muhimu kesho.