Home Habari za michezo YANGA KIFO AU UHAI DAKIKA 900 ZA MWISHO KUAMUA TAJI

YANGA KIFO AU UHAI DAKIKA 900 ZA MWISHO KUAMUA TAJI

0

LICHA ya kuongoza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa tofauti ya alama tano, Yanga imeingia katika kipindi kigumu zaidi cha msimu wa 2025/26 ikiwa imebakiza mechi 10 ambazo zitaamua moja kwa moja hatma ya kutetea ubingwa wao.

Kwa mabingwa hao watetezi, kila mchezo uliosalia ni kama fainali. Presha inaongezeka kadri msimu unavyokaribia ukingoni, hasa baada ya wapinzani wao wakuu Simba kurejea kwenye ubora na kuanza kukusanya pointi muhimu katika kila mchezo.

Wananchi hawana nafasi ya kufanya makosa. Ushindani mkali kutoka kwa Simba, waliopo nafasi ya pili wakiwa na alama 43 na tofauti ya pointi tano pekee, unaifanya kila alama kuwa na uzito mkubwa katika mbio za ubingwa.

Mashabiki wanasubiri kuona kama taji litaendelea kubaki upande wa kijani na njano, kwa mujibu wa ratiba, Yanga wataanza mfululizo huo wa mechi kwa mchezo wa ugenini dhidi ya KMC, kabla ya kurejea nyumbani kuikaribisha Coastal Union, kisha kusafiri hadi Dodoma kuvaana na Dodoma Jiji.

Mechi hizi tatu za mwanzo zitakuwa kipimo muhimu cha uimara wa kikosi hicho, hasa baada ya sare ya Kariakoo Derby iliyoacha maswali kwa mashabiki.

Baada ya hapo, Yanga watacheza mechi mbili mfululizo za nyumbani dhidi ya Singida Black Stars na Namungo FC. Hapa presha ya kupata matokeo chanya itaongezeka zaidi, kwani alama sita zitakuwa muhimu ili kuendelea kujiimarisha kwenye mbio za ubingwa.

Kupoteza pointi katika hatua hii kunaweza kuifanya safari yao kuwa ngumu zaidi, changamoto kubwa zaidi itakuja kwenye michezo ya ugenini dhidi ya Mashujaa FC na Fountain Gate FC, viwanja ambavyo mara nyingi vimekuwa vigumu kwa timu kubwa. Matokeo ya michezo hii yanaweza kubadili kabisa mwelekeo wa mbio za ubingwa.

Miongoni mwa michezo itakayovuta hisia za wengi ni ule wa nyumbani dhidi ya Azam FC, unaotarajiwa kuwa kama β€œfainali kabla ya fainali.” Ubora wa vikosi vyote viwili unaufanya mchezo huu kuwa na uzito mkubwa katika kuamua hatma ya taji.

Katika hatua ya mwisho ya msimu, Yanga wataikaribisha Tanzania Prisons kabla ya kufunga pazia kwa mchezo wa ugenini dhidi ya JKT Tanzania.

Hizi zitakuwa mechi za mwisho zenye uwezo wa kuthibitisha mafanikio au kuvunja ndoto ya kutetea ubingwa.

Ili kujihakikishia ubingwa bila kutegemea matokeo ya wapinzani wao, Yanga wanahitaji kushinda mechi zote 10 zilizosalia na kufikisha alama 30 muhimu.

Safari hii si ya ushindani pekee, bali ni vita inayohitaji umakini, nidhamu na uthabiti wa hali ya juu ili kuepuka kupoteza pointi muhimu katika hatua hii ya mwisho ya msimu.