UONGOZI wa klabu ya Simba huenda ukalazimika kufungua pochi mapema katika dirisha lijalo la usajili, ukilenga kuwania saini ya mshambuliaji wa Medeama, Salim Adams, kwa sasa ameibuka kuwa gumzo kutokana na kiwango chake bora.
Nyota huyo anayekipiga Ligi Kuu ya Ghana ameendelea kuwa tishio kubwa kwa mabeki kila anaposhuka uwanjani, akifunga mabao ya aina mbalimbali na kuwaumiza wapinzani bila huruma, jambo linalowapa presha hata timu kubwa barani Afrika.
Taarifa zinaeleza kuwa Simba wamekuwa wakimfuatilia kwa karibu tangu mwanzo wa msimu kupitia skauti wao, na kadri muda unavyokwenda ndivyo kiwango chake kinavyozidi kupanda na kuwavutia zaidi. Wiki hii pekee amefunga mabao mawili, akizidi kujiimarisha kwenye orodha ya vinara wa ufungaji nchini humo.
Uwezo wake wa kumalizia nafasi ndiyo silaha yake kubwa ana nguvu kwenye mipira ya juu, ana shuti kali la mguu wa kushoto, na ana akili ya kipekee ya kujipanga eneo sahihi kwa wakati muafaka.
Kutokana na makali hayo, baadhi ya makipa wa Ghana wamembatiza jina la ‘jambazi sugu’, wakimaanisha kuwa anapopata hata nafasi ndogo, huwa hana masihara.
Staili yake ya uchezaji pia inaelezwa kufanana na baadhi ya washambuliaji hatari waliowahi kupita ndani ya kikosi cha Simba.
Simba wanakabiliwa na ushindani mkali katika mbio za kuwania saini yake, kwani kiwango chake kimeanza kuvutia klabu kutoka Afrika Kaskazini pamoja na Ulaya. Kila bao analofunga linaongeza thamani yake sokoni, hivyo uongozi wa Simba unapaswa kufanya maamuzi ya haraka kabla dili hilo halijawa gumu zaidi kukamilika.