Home Habari za michezo MECHI YA MOTO KESHO, SIMBA YATAKA KUZIDI KUWAPA PRESHA YANGA

MECHI YA MOTO KESHO, SIMBA YATAKA KUZIDI KUWAPA PRESHA YANGA

0

KUELEKEA mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kesho, Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, ameweka wazi msimamo wa kikosi chake, akisisitiza kuwa wamejiandaa kikamilifu kwa ajili ya pambano hilo muhimu dhidi ya JKT Tanzania.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa saa 12:15 jioni katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, ambapo Simba watakuwa wenyeji wakiiwakaribisha JKT Tanzania kwenye pambano linalosubiriwa kwa hamu.

Akizungumzia maandalizi ya timu yake, Barker amesema wanautambua ubora wa wapinzani wao na hawapo tayari kuwadharau, akisisitiza kuwa kila timu inayoshiriki Ligi Kuu ina uwezo wa kufanya matokeo ya kushangaza.

β€œTumejiandaa vizuri kuwakabili JKT Tanzania huku tukiheshimu uwezo wao. Tutacheza kwa nidhamu kubwa na umakini, hatutawaona wapinzani wetu kama wanyonge, hasa katika kipindi hiki muhimu cha ligi,” amesema Barker.

Kocha huyo ameongeza kuwa dhamira ya Simba katika mechi zilizosalia ni kushinda kila mchezo na kuhakikisha hawapotezi alama, akibainisha kuwa ushindi ni jambo lisilo na mjadala kwa sasa.

β€œLengo letu ni kushinda michezo yote iliyobaki. Hatutaki kupoteza alama hata moja,” amesisitiza.

Kauli hiyo inakuja wakati mbio za ubingwa zikiwa zimepamba moto, huku Yanga wakiongoza msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi tano.

Hali hiyo inaifanya Simba kutokuwa na nafasi ya kufanya makosa, kwani kila alama tatu ni muhimu katika harakati za kuendelea kuweka presha kwa watani wao wa jadi na kudumisha matumaini ya kutwaa ubingwa.