KIUNGO mshambuliaji wa Yanga SC, Duke Abuya, ameingia kwenye gumzo kubwa baada ya taarifa kueleza kuwa amekubali kuongeza mkataba mpya wa kuendelea kusalia ndani ya kikosi hicho kwa msimu ujao.
Uamuzi huo unatajwa kuja kufuatia mazungumzo yaliyoendeshwa kwa kina kati ya menejimenti ya klabu hiyo na upande wa mchezaji, yakilenga kuimarisha mustakabali wa timu hiyo yenye malengo makubwa ya ndani na kimataifa.
Awali, hatma ya Abuya ilikuwa haijawa wazi kutokana na kuvutiwa na klabu mbalimbali, huku Azam FC ikitajwa kuwa miongoni mwa timu zilizokuwa zikifuatilia kwa karibu saini yake.
Hali hiyo ilizua taharuki kwa mashabiki wa Yanga waliokuwa na hofu ya kumpoteza mmoja wa viungo wao muhimu katika kikosi.
Licha ya presha hiyo ya uhitaji kutoka kwa timu nyingine, inaelezwa kuwa Abuya ameona ni vyema kuendelea kubaki Jangwani, akivutiwa na mradi wa timu pamoja na mazingira ya ushindani aliyoyazoea.
Kiungo huyo amekuwa na mchango mkubwa ndani ya kikosi hicho, hasa katika ubunifu wa mashambulizi na uthabiti wa safu ya kiungo.
Kwa sasa, hatua hiyo inaonekana kuwa ni pigo kwa klabu zilizokuwa zikimnyemelea, huku ikiwa ni habari njema kwa mashabiki wa Yanga wanaotarajia kuona mwendelezo wa kiwango chake msimu ujao.
Endapo makubaliano hayo yatakamilika rasmi, basi Yanga itakuwa imejihakikishia kubaki na silaha muhimu katika harakati zake za kutetea ubingwa na kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa.