WAKATI Simba ikishuka dimbani leo kusaka alama tatu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya JKT Tanzania, pambano hilo linatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mwenge.
Kuelekea mchezo huo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema hawatarajii kazi nyepesi kutokana na ubora wa wapinzani wao.
Ameeleza kuwa JKT Tanzania imeonyesha ushindani mkubwa msimu huu, jambo linaloifanya kuwa miongoni mwa timu bora kwa sasa kulingana na msimamo wa ligi, ikishika nafasi ya nne nyuma ya vinara, Simba na Azam FC.
βUkiangalia mwenendo wao, JKT Tanzania si timu ya kubeza. Ni timu ambayo imekuwa na kiwango kizuri na imepoteza mechi chache sana hadi sasa,β amesema.
Ameongeza kuwa takwimu zinaonyesha ugumu wa mpinzani huyo, akibainisha kuwa wamepoteza michezo minne tu kati ya 20 waliocheza, hali inayothibitisha uimara wao.
Kutokana na hali hiyo, Ahmed amesema Simba inalazimika kuingia uwanjani kwa tahadhari kubwa, ikitambua kuwa mchezo huo utakuwa mgumu na wenye ushindani wa hali ya juu.
βNi mechi ngumu, mechi ya ushindani mkubwa. Tunapaswa kuwa makini na kucheza kwa umakini mkubwa ili kupata matokeo chanya,β amesisitiza.
Amegusia suala la uwanja, akieleza kuwa licha ya Simba kuwa ugenini kiasili, mazingira ya Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo yanaifanya JKT Tanzania kuwa na faida zaidi kama wenyeji.
Simba inaingia katika mchezo huo ikiwa na lengo la kupata ushindi, lakini ikitambua wazi kuwa haitakuwa kazi rahisi mbele ya JKT Tanzania iliyo kwenye kiwango kizuri msimu huu.