Home Habari za michezo CHAMA NI HATARI AIPA SIMBA POINTI TATU MUHIMU MBWENI

CHAMA NI HATARI AIPA SIMBA POINTI TATU MUHIMU MBWENI

0

SIMBA SC imeendelea kushikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni.

Katika pambano hilo lililokuwa na ushindani mkubwa, kiungo mshambuliaji Clatous Chama aliibuka shujaa wa Simba baada ya kufunga bao pekee la ushindi dakika ya 35.

Bao hilo lilitokana na kazi nzuri ya Elie Mpanzu ambaye alionesha utulivu na ubunifu mkubwa kabla ya kumtengenezea nafasi Chama kufumania nyavu.

Mchezo ulianza kwa kasi ya wastani huku timu zote zikicheza kwa tahadhari kubwa, kila upande ukijaribu kutafuta mianya ya kushambulia bila kuacha nafasi nyingi nyuma.

Licha ya juhudi hizo, hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kuongeza bao, na kuifanya Simba kwenda vyumbani ikiwa mbele kwa bao hilo moja.

Kipindi cha pili kilishuhudia JKT Tanzania wakiongeza nguvu wakisaka bao la kusawazisha, lakini uimara wa safu ya ulinzi ya Simba uliendelea kuwa kikwazo.

Simba nao walionekana kucheza kwa nidhamu wakilinda ushindi wao huku wakitumia mashambulizi ya kushtukiza kutafuta bao la pili, ambalo hata hivyo halikupatikana.

Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha alama 46 na kuendelea kubaki nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, huku Azam FC wakishuka hadi nafasi ya tatu wakiwa na pointi 43.

Kwa upande wake, Clatous Chama anaendelea kuthibitisha ubora wake msimu huu, akiendelea kuwa mhimili muhimu katika safu ya ushambuliaji ya Simba na tishio kwa mabeki wa timu pinzani kila anapokanyaga dimbani