Home Habari za michezo KOCHA PEDRO ATIMULIWA RASMI YANGA SC

KOCHA PEDRO ATIMULIWA RASMI YANGA SC

0

UONGOZI wa Klabu ya Yanga SC umetibua hali ya hewa ya soka la Tanzania baada ya kutangaza rasmi kumfuta kazi Kocha Mkuu, Pedro Gonçalves.

Taarifa hiyo, iliyotolewa na Mtendaji Mkuu wa klabu, imekuja ghafla na kuwaacha mashabiki wa Wananchi wakiwa na mshangao mkubwa.

Kupitia kurasa rasmi za klabu, Yanga imemshukuru kocha huyo raia wa Ureno kwa mchango wake ndani ya timu na kumtakia kila la heri katika majukumu yake yajayo.

Hata hivyo, taarifa hiyo haikuweka wazi sababu za uamuzi huo, jambo lililoibua maswali mengi miongoni mwa wadau wa soka.

Uamuzi huo unafuatia matokeo ya hivi karibuni, ikiwemo sare ya mabao 2-2 dhidi ya watani wao Simba SC katika dabi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa Jumapili iliyopita.

Licha ya Yanga kuonyesha moyo wa kupambana kwa kusawazisha mabao mawili, inaonekana matokeo hayo hayakutosha kumuweka salama Gonçalves.

Kwa kipindi cha hivi karibuni, kocha huyo alikuwa akikabiliwa na presha kubwa kutoka kwa baadhi ya mashabiki, waliokuwa wakikosoa mtindo wa uchezaji wa timu pamoja na matokeo yasiyoridhisha katika baadhi ya michezo.

Kufuatia kuondoka kwake, jukumu la kuiongoza timu limekabidhiwa kwa makocha wasaidizi, Abdihamid Moalin na Patrick Mabedi, ambao wataisimamia hadi mwisho wa msimu. Wawili hao wanatarajiwa kubeba dhamana nzito ya kuhakikisha timu inabaki kwenye ushindani wa ubingwa wa Ligi Kuu pamoja na michuano mingine.

Kuondoka kwa Pedro kunaashiria mwisho wa sura moja ndani ya Yanga na mwanzo wa ukurasa mpya, huku macho ya mashabiki yakielekezwa kuona nini kitafuata katika safari ya klabu hiyo kongwe.