Home Habari za michezo SIMBA WAJIPANGA MAPEMA, WAMCHOMOA NYOTA ZAM BURE

SIMBA WAJIPANGA MAPEMA, WAMCHOMOA NYOTA ZAM BURE

0

IMEELEZWA kuwa uongozi wa klabu ya Simba SC umeanza rasmi mchakato wa usajili kuelekea msimu wa 2026/27, kwa kulenga kumsajili beki wa kulia wa Azam FC, Nathaniel Chilambo.

Simba inaonekana kuanza mapema maandalizi ya msimu ujao, hatua inayodhihirisha dhamira ya kujijenga upya kwa ushindani mkubwa. Mchakato huo unaendeshwa kwa kuzingatia mapendekezo ya benchi la ufundi linaloongozwa na kocha mkuu, Steve Barker, likitathmini maeneo yenye uhitaji wa kuimarishwa ndani ya kikosi.

Taarifa zinaeleza kuwa tayari mazungumzo yamefanyika na kufikia makubaliano ya awali (pre-contract) kati ya pande hizo mbili, ambapo Chilambo anatarajiwa kujiunga na Simba mara tu mkataba wake na Azam FC utakapomalizika mwishoni mwa msimu huu.

Chanzo cha habari kimeeleza kuwa kwa muda mrefu nafasi ya beki wa kulia imekuwa ikitajwa kuhitaji ushindani zaidi ndani ya kikosi cha Simba, hivyo ujio wa Chilambo unaonekana kuwa suluhisho sahihi la kuziba pengo hilo.

Mbali na hilo, beki huyo anasifiwa kwa kasi, nidhamu ya hali ya juu pamoja na uwezo mkubwa wa kusaidia mashambulizi na kurejea kwa haraka kujilinda, sifa zinazomfanya kuwa mchezaji wa kisasa katika nafasi hiyo.

Chilambo ameonyesha kiwango bora katika Ligi Kuu Tanzania Bara, hali iliyomuweka miongoni mwa mabeki wa kulia wanaong’ara na kuvutia macho ya vigogo mbalimbali, akiwemo Simba ambao wamevutiwa na uwezo wake hadi kuafikiana na benchi la ufundi kuhusu ujio wake.

Kutokana na mkataba wake kumalizika mwishoni mwa msimu huu, Simba inalenga kunufaika na fursa hiyo kwa kumsajili bila gharama ya usajili, mbinu inayotumiwa na klabu nyingi kubwa duniani ili kuepuka ushindani mkali wa dirisha rasmi.

Iwapo mipango hiyo itakamilika kama ilivyopangwa, Chilambo ataanza rasmi kuitumikia Simba SC kuanzia Julai 2026.

Usajili huu unaashiria namna Simba inavyojipanga kwa mapambano ya msimu ujao, huku jukumu kubwa likibaki kwa benchi la ufundi kuhakikisha wanaitumia ipasavyo nguvu na ubora wa nyota huyo mpya ndani ya kikosi.