Home Habari za michezo ABDURAZACK MWENGA AKACHA GEREJI,SOKA APANDA ULINGONI AIOMBA RADHI TPBRC

ABDURAZACK MWENGA AKACHA GEREJI,SOKA APANDA ULINGONI AIOMBA RADHI TPBRC

0

KATIKA mitaa ya Mabibo na Manzese jijini Dar es Salaam, maisha ni mchakamchaka wa kutafuta shilingi ili mkono uende kinywani.

Hata hivyo, hapo, mchezo wa ngumi siyo burudani tu, bali ni njia ya kujiondoa kwenye umasikini.

Miongoni mwa vijana walioamua kuvaa glavu na kuingia ulingoni kusaka heshima na riziki ni Abdurazack Mwenga, bondia wa uzito wa Super Light ambaye kwa sasa anapitia kipindi kigumu cha kutumikia kifungo cha mwaka mmoja kutojihusisha na ngumi baada ya kufanya vurugu huku akikataa kushuka ulingoni.

Tukio hilo ambalo limemfanya kukaa kifungoni, anasema ni miongoni mwa mambo yanayomuumiza huku akiwa ametumikia kwa takribani miezi miwili sasa tangu afungiwe Machi mwaka huu.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na bondia huyo mwenye umri wa miaka 31 kufahamu maisha yake kuanzia utoto, changamoto za nje ya ulingo na kilio chake kwa mamlaka za ngumi akiomba kufunguliwa ili aendelee kupambania kipaji chake.

REKODI ZAKE

Mwenga ni bondia wa kulipwa nchini Tanzania mwenye rekodi ya mapambano 13, ingawa ni 10 pekee yaliyopo kwenye rekodi rasmi za BoxRec.

Katika rekodi hizo za mapambano 10 tangu Novemba 3, 2023, ameshinda matatu (mawili kwa KO), amepoteza manne, na sare tatu.

Kwa mujibu wa Boxrec, mtandao unaotunza takwimu za mabondia dunia, Mwenga anashika nafasi ya 25 kati ya mabondia 121 wa uzito wa Super Light hapa Tanzania, huku duniani akijitafuta katika nafasi ya 820 kati ya mabondia 2,677 jambo ambalo anaamini kama atarudi kwenye ubora alioanza nao anaweza kuzivunja na kuandika rekodi kubwa zaidi.

“Nimecheza mechi 13 lakini 10 zipo kwenye BoxRec na naamini kama ningeendelea kucheza basi sasa hivi ningekuwa mbali kwenye rekodi za dunia lakini naendelea kujiandaa hadi nitakapofunguliwa, naamini nitaonyesha uwezo wangu,” anasema Mwenga.

NDONDI ZA MASIKINI

Mwenga anasema ngumi ni mchezo wa watu wa hali ya chini kwa sababu ni wa kuumizana ambao mwenye fedha hawezi kuu ch eza kwa kuutaka.

“Si dhani kama wewe leo hii mtu na pesa zako halafu ukasema nataka kupigana na kuhatarisha maisha, ni ngumu kwa kweli, wengi ambao tunacheza ngumi ni watu wa hali ya chini,” anasema Mwenga.

Akihusisha na maisha ya Mabibo, Mwenga anasema: “Mabibo maisha yetu sisi utumbo, miguu ya kuku kawaida… Yaani hiyo ndio mboga hasa ndio sikukuu yaani ukisikia ugali na miguu ya kuku ni sikukuu nyumbani, sasa kwa mabondia hatufuati ule mlo anaotakiwa kula bondia ili aweze kuwa vizuri, sasa si umasikini huo,” anasimulia.

“Ni kitu cha kujivunia kwa kweli kwa sababu kuna mabondia wengi wanaofanya vizuri kitaifa na kimataifa wanatokea Mabibo na Manzese.”

UTOTO WAKE

Anasema mambo ya ngumi alianza tangu akiwa utotoni kwani alikuwa mtoto mtukutu kiasi cha kutumia marungu kupigana mitaani badala ya kutumia mikono.

Shuleni nako hakuwa vizuri, aliingia saa nne na kutoka saa sita bila kuulizwa. Furaha yake kubwa ilikuwa ni kuchonganisha wenzake wapigane huku yeye akigeuka kuwa refa.

“Nilianza mambo ya ngumi tangu nikiwa mdogo kabisa, maana nilikuwa mtoto mtukutu sana. Badala ya kupigana kwa mikono, nilikuwa natumia hadi marungu mitaani. Hata shule sikuwa na utulivu, naweza kuingia saa nne na kutoka saa sita bila hata kuulizwa,” anasema Mwenga.

“Ukweli ni kwamba, furaha yangu kubwa ilikuwa kuwachonganisha wenzangu wapigane, halafu mimi nageuka refa nikisimamia pambano lao. Hapo ndipo ninapoona kabisa chanzo cha mimi kuwa bondia kilianzia.”

MECHI YA KWANZA

Mwenga anakumbuka siku yake ya kwanza kupanda ulingoni, alikuwa muoga akauona ulingo ni mkubwa kama Uwanja wa Benjamin Mkapa.

“Nilikuwa na kilo 63, mpinzani wangu alikuwa na kilo 69, kiukweli ilikuwa ngumu sana lakini nilipambana hadi mwisho, nikashinda,” anasema.

MACHOZI YA MKEWE

Anasema anapata sapoti kubwa kutoka kwa familia yake hasa mkewe lakini anakumbuka mwaka 2023 alipigwa hadi kutoa kamasi, kisa kilichomfanya mkewe kukataa kwenda ulingoni kumtazama.

“Ni wiki nzima mke wangu alikuwa na mawazo, hicho ndio kilimfanya awe na kinyongo cha kutotaka kwenda tena ulingoni nikiwa nacheza anaishia kuangalia labda kwenye TV tu,” anabainisha.

Aidha anasema jeraha lililowahi kumweka nje muda mrefu aliwahi kuvunjika mbavu mazoezini mwaka 2021-2022 wakati akijiandaa na pambano, hali iliyomwweka nje ya mchezo kwa miezi nane.

MAREFA CHANGAMOTO

Kilio chake kikubwa ni dhuluma kutoka kwa majaji na marefa. Anadai kuna upendeleo wa kimaeneo yanayoharibu haki ya bondia na mchezo wa ngumi kwa jumla.

“Ushauri wangu viongozi wa Chama cha Ngumi, BMT na Serikali kijumla watizame majaji na marefa wafanye kazi kwa uweledi, tupigane kweli mtu akipigwa kapigwa, akishinda akashinda,” anasisitiza.

“Kuna utaratibu wa ajabu hasa kwa marefa wanapochezesha mapambano makubwa kama ya kina Hassan Mwakinyo wanachezesha vizuri ila huku chini ni kama wanadharau kwa sababu hawatendi haki.”

Hata hivyo, anapongeza Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TBRC) kwa kusimamia afya za mabondia, akisema sasa wanapimwa homa ya ini, figo na presha kabla ya mapambano, tofauti na zamani.

MASILAHI NA MAISHA YA MAKOCHA

Mwenga anafichua kuwa ngumi bado hazijamlipa vilivyo na pambano lililompa fedha nyingi zaidi lilikuwa la Kenya alilipwa Sh450,000.

Anasema mchezo wa ngumi kwa Tanzania bado haujapata wadhamini wa kutosha akijitolea mfano yeye kuwa analipwa Sh150,000 kwenye pambano ambalo ukija kupiga hesabu inaishia kwenye maandalizi.

“Napewa Sh150,000, yaani napewa leo inaishia kwenye maandalizi tu… Ukirudi nyumbani una Sh20,000 mkeo anakukanda uso unamwambia hii shika kanunue kijora, maisha yanaendelea,” anasimulia.

Anasema fedha hiyo haitoshelezi hata kumpa hela ya soda makocha wanaowasimamia na kupitia wakati mgumu wa kuwatengeneza mabondia.

“Wanakula majasho yetu, wanakula mikamasi yetu, kocha anakwambia ‘jabu’ ukipiga jasho limemdondokea mdomoni, lakini hakuna wanachopata kutokana na pesa ambayo tunalipwa kwenye mapambano, makocha wanastahili kupewa kipaumbele sana,” anasema.

SABABU YA KUFUNGIWA

Mwenga amefungiwa mwaka mmoja hadi Machi 28, 2027, kufuatia kugoma kushuka ulingoni akipinga matokeo ya pambano alilodai kuonewa.

Hiyo ilikuwa Machi 26, 2026 jijini Dar es Salaam alipopanda ulingoni kupambana na Wazir Magombana na kupoteza kwa pointi.

Katika pambano hilo, kwa mujibu wa Boxrec, majaji wote watatu walimpa ushindi Magomba ambapo wote walitoa alama 60, huku wakimpa Mwenga 54.

Bondia huyo anaomba radhi kwa Kamisheni ya Ngumi za kulipwa Tanzania (TPBRC) na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kutokana na kitendo alichokifanya.

“Naomba wanifungulie ili niweze kupigana, inanikwamisha kwenye ndoto zangu,” anasema.

SOKA

Kabla ya ngumi, Mwenga alikuwa akicheza mpira wa miguu nafasi ya beki wa kulia akishiriki Ligi Daraja la Tatu akiwa na timu ya FC Tabora. Mwaka 2010 alifanikiwa kushiriki mashindano ya UMISETA. Lakini baadaye aliamua kuacha mpira wa miguu kwa sababu aliona kuna watu wenye uwezo mkubwa zaidi yake, akaamua kuelekeza nguvu zake kwenye ndondi.

Anasema yeye ni shabiki mkubwa wa Yanga kwa Tanzania na nje ni Manchester United.

MALENGO YAKE

Bondia huyo anasema ana malengo makubwa ya kushinda mikanda ya WBC na WBO na kuwa bondia anayetajwa duniani kama Floyd Mayweather, Mike Tyson, au Gervonta Davis.

Anaamini akifunguliwa, ndani ya kipindi cha miaka miwili atafikia kiwango hicho cha dunia na kutimiza malengo yake ambayo kwa watu wanaweza wasiamini ila kwake inawezekana.

“Mimi nina malengo makubwa na nilijiwekea mapema lakini adhabu imeniharibia, naamini kwa uwezo wangu nitafikia kile ninachokikusudia kwa sababu nina kiwango,” anasema Mwenga ambaye nje ya ngumi ana ujuzi wa ufundi wa magari, fani aliyoisomea kabla hata hajaingia kwenye mchezo huo.