Home Habari za michezo NAMBA ZINAIKATAA KMC

NAMBA ZINAIKATAA KMC

0

IKIWA ipo mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikikusanya pointi tisa baada ya mechi 21, KMC sasa inaingia kwenye vita ya mwisho ya kujiokoa isishuke daraja zikisalia mechi tisa ambazo zinaonekana kuwa fainali kwa vijana hao wa Kinondoni.

KMC ndiyo timu iliyoshinda mechi chache zaidi Ligi Kuu Bara msimu huu ambazo ni mbili dhidi ya Mashujaa na Dodoma Jiji kwa bao 1-0 katika kila mchezo.

Pia KMC ndiyo timu iliyokusanya pointi chache zaidi ambazo ni tisa zilizotokana na kushinda mechi mbili na sare tatu. Wakati huohuo, KMC ndiyo timu iliyopoteza mechi nyingi zaidi zikifika 16 na ndiyo iliyoruhusu mabao mengi zaidi ambayo ni 32 na kufunga machache 8. Kitu pekee ambacho KMC inalingana na timu zingine, ni idadi ya mechi ambazo ni 21.

Takwimu hizo zinaonyesha wazi ukubwa wa kazi waliyonayo katika kipindi hiki cha mwisho cha msimu.

Kwa hesabu za kawaida za ligi, timu nyingi zinazobaki salama mara nyingi hukusanya angalau pointi 30 hadi 35 mwishoni mwa msimu. Hii ina maana KMC italazimika kufanya kitu kikubwa ndani ya mechi tisa zilizobaki ili kufikia eneo salama.

Kwa sasa, KMC ina pointi tisa huku nafasi ya 14 inayoshikiliwa na Mbeya City ikiwa na pointi 21. Tofauti ya pointi 12 ikiwa zimebaki mechi chache inaifanya kila mechi KMC kuhitaji ushindi.

KMC inaweza kufikisha kiwango cha juu cha pointi 36 kama itashinda mechi zote tisa zilizobaki. Hata hivyo, kutokana na mwenendo wao wa msimu mzima, hilo linaonekana kuwa jambo gumu sana kutokea.

Hesabu zinaonyesha KMC ikipoteza mechi tano kati ya tisa zilizobaki, hata ikishinda zote nne zilizobaki itafikisha pointi 21 pekee. Pointi hizo zinaweza zisitoshe kabisa kuinasua kutoka eneo la kushuka daraja.

Hatari zaidi ipo kwenye uwezekano wa kupoteza mechi sita. Hapo KMC itabakiwa na nafasi ya kufikisha pointi 18 tu kama itashinda mechi tatu zilizobaki, jambo ambalo karibu linaifanya ishuke daraja mapema.

Ratiba yao pia haionekani kuwa rafiki. Bado wanakutana na vigogo wawili wa ligi, Azam na Simba huku pia wakiwa na mechi ngumu dhidi ya TRA United na Mashujaa.

Mechi zinazoweza kubeba matumaini yao ni zile dhidi ya Fountain Gate, Mtibwa Sugar, Coastal Union na Namungo ambazo zote zinapambana kwenye ukanda wa chini.

Kitu kingine kinachowaumiza KMC ni safu yao ya ushambuliaji. Wamefunga mabao manane pekee katika mechi 21, idadi ndogo zaidi ligi nzima. Takwimu hiyo inaonyesha kwanini wamekuwa wakipata shida kubadili sare au vipigo kuwa ushindi.

Ukuta wao bado haujawa imara baada ya kuruhusu mabao 32, wastani wa zaidi ya bao moja kwa kila mchezo. Katika hatua kama hii ya msimu, tofauti ndogo tu kwenye safu ya ulinzi inaweza kuamua hatima ya timu.

Kwa sasa, picha halisi inaonyesha KMC haina nafasi ya kufanya makosa mengi tena. Kila kipigo kinaisogeza karibu zaidi kwenda Ligi ya Championship na kama haitabadilika, huenda ikawa timu ya kwanza kushuka daraja kabla msimu haujafika mwisho.

Mechi za KMC zilizobaki ni dhidi ya Fountain Gate (Mei 10, nyumhani), Mtibwa Sugar (Mei 14, ugenini), Pamba Jiji (Mei 20, nyumbani), Azam (Mei 25, ugenini), TRA United (Juni 12, nyumbani), Coastal Union (Juni 15, ugenini), Namungo (Juni 24, nyumbani), Mashujaa (Juni 27, ugenini) na Simba (Juni 30, ugenini).

Wakati huohuo, KMC ambayo imetoka kuchapwa bao 1-0 na Yanga, kuna kitu beki wa kikosi hicho, Mudathir Nassor kuhusu washambuliaji wa mabingwa hao watetezi.

Nassor amesema pamoja na KMC kupoteza nyumbani kwa bao 1-0 dhidi ya Yanga, lakini hakukuwa na ugumu mkubwa kuwazuia washambuliaji wa wapinzani hao kutokana na aina yao ya uchezaji kufanana.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mudathir amesema aliweza kuwasoma vizuri washambuliaji wa Yanga, Prince Dube na Laurindo Aurelio ‘Depu’ jambo lililomsaidia kutowapa nafasi ya kufanya madhara makubwa langoni mwa KMC.

“Hakuna ugumu wa kuwakaba washambuliaji wa Yanga kwa sababu aina yao ya uchezaji inafanana ndio maana niliweza kuwasoma vizuri na kutowapa uhuru,” amesema Mudathir.

Beki huyo alieleza kuwa, changamoto kubwa kwa upande wa KMC haikuwa kufika langoni mwa wapinzani, bali kushindwa kutumia nafasi walizozitengeneza kwenye eneo la ushambuliaji.

“Ubora wetu ulikuwa kwenye kutengeneza nafasi na sio kwamba tulikuwa hatufiki langoni kwa Yanga, tulikuwa tunafika ila hatukuwa na ubora kwenye eneo la mbele,” amesema.

Mudathir alieleza kuwa, hakuna mchezaji anayefurahia kufungwa, huku akibainisha kwamba KMC itaendelea kupambana kuhakikisha inabaki salama kwenye ligi.

“Matokeo yanatuumiza, hakuna anayependa kufungwa. Tutaendelea kupambana, tukishuka haya, tukisalia basi itakuwa jambo la kheri, lakini kikubwa kwa sasa tunapambana,” amesema.

Aidha, beki huyo amesema michezo mikubwa ya aina hiyo inaendelea kumpa uzoefu kutokana na kuwa huu ni msimu wake wa kwanza ndani ya KMC tangu alipojiunga na timu hiyo katika dirisha dogo Januari 2026 akitokea Zimamoto ya Zanzibar.