Home Habari za michezo OKELLO AFUNGUKA SIRI YA USHINDI WA YANGA DHIDI YA KMC

OKELLO AFUNGUKA SIRI YA USHINDI WA YANGA DHIDI YA KMC

0

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Allan Okello amesema ushindi wa bao 1-0 walioupata dhidi ya KMC haukuwa rahisi licha ya timu yake kutengeneza nafasi nyingi za kufunga, hasa kipindi cha kwanza cha mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Okello ambaye ndiye aliyefunga bao pekee la ushindi, amesema Yanga ilianza mchezo kwa kasi na kutawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza, lakini ukosefu wa umakini kwenye umaliziaji uliwafanya washindwe kutumia nafasi walizozipata.

Amesema kutokana na nafasi walizozalisha, walipaswa kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa angalau mabao matatu, jambo lililosababisha hali ya huzuni na majuto kwa baadhi ya wachezaji ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo wakati wa mapumziko.

Nyota huyo raia wa Uganda amesema kipindi cha pili kilikuwa tofauti baada ya KMC kuongeza umakini mkubwa kwenye safu yao ya ulinzi na kuziba mianya mingi ambayo Yanga ilikuwa ikiitumia kushambulia katika dakika za mwanzo za mchezo.

Kutokana na mabadiliko hayo, Okello amesema walilazimika kubadili mbinu kwa kujaribu mashuti ya mbali pamoja na kusubiri nafasi chache walizokuwa wakizipata ndani ya eneo la hatari, hali iliyosaidia kupata bao muhimu lililowapa pointi tatu.

Kiungo huyo ameweka wazi kuwa kwa sasa jambo kubwa kwa Yanga si mafanikio binafsi wala tuzo za mchezaji bora wa mechi, bali ni kuhakikisha timu inaendelea kukusanya ushindi katika kila mchezo wa ligi huku mbio za ubingwa zikizidi kupamba moto.

Okello amewashukuru mashabiki wa Yanga kwa kuendelea kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono timu hiyo, akieleza kuwa sapoti yao huwapa morali kubwa na kujiamini zaidi wanapokuwa uwanjani.

“Tunawahitaji mashabiki nyuma yetu kwa sababu wanatupa nguvu ya kupambana na kupata pointi tatu kila siku,” amesema Okello.