Home Habari za michezo BAADA YA PEDRO KUONDOKA, BUBA KIKAANGONI

BAADA YA PEDRO KUONDOKA, BUBA KIKAANGONI

0

MAISHA ya winga wa Yanga SC, Buba Jammeh, ndani ya kikosi hicho yanaonekana kuingia kwenye wakati mgumu baada ya kushindwa kuonyesha kiwango kilichotarajiwa tangu aliposajiliwa na mabingwa hao wa Tanzania Bara.

Nyota huyo ambaye aliwasili kwa matarajio makubwa, bado hajawa na mchango mkubwa ndani ya kikosi hicho jambo linalozua maswali kuhusu hatma yake.

Buba ni mmoja wa wachezaji waliosajiliwa katika dirisha dogo la usajili, usajili ambao ulifanyika chini ya mapendekezo ya aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Gonçalves.

Ujio wake ulitajwa kuwa sehemu ya maboresho ya kuongeza kasi na ubunifu katika safu ya ushambuliaji ya Wananchi.

Hata hivyo, tangu ajiunge na timu hiyo, winga huyo ameshindwa kuonyesha kiwango kilichowavutia viongozi na mashabiki wa Yanga.

Akipewa nafasi mara chache, Buba bado hajaweza kutumia vyema nafasi hizo kuthibitisha uwezo wake ndani ya kikosi hicho chenye ushindani mkubwa.

Kuondoka kwa kocha Pedro Gonçalves kunatajwa kuwa pigo jingine kwa mchezaji huyo, kwani ndiye aliyekuwa akimuamini na kusimamia usajili wake.

Hali hiyo imeongeza uwezekano wa nyota huyo kukosa nafasi zaidi chini ya benchi jipya la ufundi litakaloundwa kuelekea msimu ujao.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa viongozi wa Yanga wanaendelea kufanya tathmini ya kikosi chao kwa ajili ya msimu wa 2026/27, huku baadhi ya wachezaji wakitajwa kuwa kwenye hatari ya kuachwa kutokana na kutoridhisha kiuchezaji.

“Huenda msimu ujao Buba asiwe sehemu ya kikosi cha timu hiyo kwa sababu ya kushindwa kuonyesha kiwango kizuri na kushindwa kupata nafasi katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo,” kilisema chanzo cha karibu na klabu hiyo.

Iwapo Buba ataondoka mwishoni mwa msimu huu, ataungana na orodha ya wachezaji walioshindwa kudumu kwa muda mrefu ndani ya Yanga kutokana na presha ya ushindani na matarajio makubwa kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo.